Dar es Salaam
KAMATI ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania ( BoT) imeamua kuendelea na Kiwango cha Riba ya Benki Kuu (CBR) cha asilimia 6 kwa robo pili ya mwaka 2025.

Pia imesema kutokutabirika kwa sera za biashara na migogoro ya kisiasa duniani inaweza kuathiri mwelekeo wa mfumuko wa bei na ukuaji wa uchumi katika kufikia malengo yake hivyo uamuzi wa Kamati hiyo unalenga kuukinga uchumi dhidi ya athari zinazoweza kutokea kutokana na vikwazo vya kibiashara na migogoro ya kisiasa duniani.
Akitoa taarifa hiyo leo Aprili, 4 2025 jijini Dar es Salaam Naibu Gavana wa Benki Kuu Sera za Uchumi na Fedha Dk.Yamungu Kayandabila kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo Gavana Emmanuel Tutuba wakati akitoa tathimini ya mwenendo wa mwelekeo wa uchumi na mwelekeo katika robo ya pili ya mwaka 2025.
“Kwa muktadha huu, Benki Kuu itaendelea kutekeleza Sera ya fedha ili kuhakikisha riba ya mikopo ya siku saba baina ya benki inabaki ndani ya wigo wa asilimia 4-8 na mfumuko wa bei na kasi ya ukuaji wa uchumi nchini, unatarajiwa kubaki ndani ya malengo,”amesema.
Amesema riba hiyo hutoa mwelekeo wa Sera ya fedha, wenye lengo la kuhakikisha mfumuko wa bei unabaki ndani ya lengo la muda wa kati, la asilimia tano na kuchangia ukuaji endelevu wa uchumi.
Amesema katika kutathmini mwenendo wa uchumi wa dunia kwa robo ya kwanza ya mwaka 2025, Kamati ilibaini kuwa shughuli za kiuchumi katika nchi zilizoendelea na zile zinazoibukia kiuchumi ziliendelea kuimarika, na mwenendo huo unatarajiwa kuendelea katika robo zijazo za mwaka 2025.
Dk.Kayandabila amesema mfumuko wa bei ulipungua na kufikia malengo ya benki kuu za nchi nyingi duniani, kutokana na kufifia kwa athari zilizotokana na mitikisiko ya kiuchumi katika vipindi vilivyopita na utekelezaji wa sera ya fedha iliyolenga kupunguza ongezeko la ukwasi.
Ameeleza kuwa kutokana na mwenendo huo pamoja na matarajio ya kuendelea kupungua kwa mfumuko wa bei, benki kuu katika nchi nyingi zimeendelea kupunguza riba zao za Sera ya fedha na kutokutabirika kwa sera, vikwazo vya kibiashara baina ya nchi hususan zile zilizoendelea na zinazoibukia kiuchumi, pamoja na migogoro ya kisiasa vinaweza kuathiri matarajio ya ukuaji wa uchumi na kuchochea kuongezeka kwa mfumuko wa bei duniani.

Amesema katika kutathmini mwenendo wa uchumi wa dunia kwa robo ya kwanza ya mwaka 2025, Kamati ilibaini kuwa shughuli za kiuchumi katika nchi zilizoendelea na zile zinazoibukia kiuchumi ziliendelea kuimarika, na mwenendo huu unatarajiwa kuendelea katika robo zijazo za mwaka 2025.
Aidha amsema ukuaji wa uchumi unakadiriwa kufikia asilimia 5.5, katika robo ya kwanza ya mwaka 2025 na uchumi wa Zanzibar ulikua kwa asilimia 7.2 katika robo ya nne ya mwaka 2024, kutoka asilimia 2.2 katika kipindi kama hicho mwaka 2023, ukichangiwa zaidi na shughuli za malazi na chakula, ambazo kwa kiwango kikubwa huambatana na shughuli za utalii, pamoja na biashara.
Dk.Kayandabila amesema mfumuko wa bei ulikuwa tulivu sambamba na matarajio, kutokana na utekelezaji thabiti wa sera ya fedha na bajeti, uwepo wa chakula cha kutosha nchini pamoja na kupungua kwa bei za nishati duniani ambapo mfumuko wa bei ulipungua kufikia wastani wa asilimia 3.1 mwaka 2024, ukilinganishwa na wastani wa asilimia 3.8 mwaka 2023, chini ya lengo la nchi la chini ya asilimia 5, na ndani ya vigezo vya mtangamano wa kiuchumi kwa nchi za SADC na EAC.
Amefafanua katika robo ya kwanza ya mwaka 2025, mfumuko wa bei kwa Tanzania Bara ulikuwa wastani wa asilimia 3.2 na kwa upande wa Zanzibar, mfumuko wa bei ulipungua kufikia asilimia 5.1 mwaka 2024, kutoka asilimia 6.9 mwaka 2023 huku mfumuko wa bei ulipungua hadi asilimia 4.8 mwezi Februari 2025 kutoka asilimia 5.3 mwezi Januari 2025, kutokana na kupungua kwa bei za chakula.
Amesema Mfumuko wa bei unatarajiwa kuendelea kuwa tulivu, ukiwa takribani asilimia 3.2 kwa robo ya pili ya mwaka 2025 na Ujazi wa fedha ulikua imara, kwa zaidi ya asilimia 12 mwaka 2024, sanjari na utelekezaji wa sera ya fedha sambamba na ukuaji wa ujazi wa fedha ulichangiwa zaidi na ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi.
“Katika robo ya kwanza ya mwaka 2025, ukuaji wa ujazi wa fedha uliongezeka sambamba na kuimarika kwa ukwasi na mikopo kwa sekta binafsi ilikua kwa wastani wa asilimia 12.7, ambapo sehemu kubwa ya mikopo ilielekezwa kwenye shughuli binafsi hususan biashara ndogo na za kati, ikifuatiwa na shughuli za kilimo, biashara na uzalishaji viwandani,”ameeleza.
Pia alisema sekta ya fedha imeendelea kuwa imara na thabiti, ikiwa na ukwasi wa kutosha, yenye kutengeneza faida, na mtaji wa kutosha kukabiliana na mitikisiko ya kiuchumi na ubora wa rasilimali za mabenki uliendelea kuwa wa imara, ambapo uwiano wa mikopo chechefu (NPLs) ulikuwa asilimia 3.6 mwezi Februari 2025, chini ya kiwango kinachokubalika cha chini ya asilimia 5 katika Utekelezaji wa sera ya bajeti katika robo ya tatu ya mwaka 2024/25, ulikuwa wa kuridhisha.
Mapato ya kodi kwa Tanzania Bara na Zanzibar yalifikia lengo kama ilivyokuwa katika robo mbili zilizotangulia, kutokana na kuimarika kwa ufanisi na usimamizi wa kodi. Matumizi ya Serikali yaliendelea kufanyika kuendana na rasilimali zilizopo.
“Kutokana na mwenendo huu, pamoja na matarajio ya kuendelea kupungua kwa mfumuko wa bei, benki kuu katika nchi nyingi zimeendelea kupunguza riba zao za Sera ya fedha,”amesema.
Vilevile amesema Kamati ilibaini kuwa toka ilipokutana katika kikao chake cha Januari 2025, mwenendo wa uchumi nchini umeendelea kuimarika na matarajio ni kuwa imara hivyo kuimarika kwa uchumi nchini kunathibitishwa na matokeo ya tafiti za mtazamo wa soko na maoni ya wakurugenzi watendaji wa makampuni mbalimbali nchini kuhusu mwenendo wa uchumi zilizofanyika Februari 2025.
Amesema mwelekeo huu pia unathibitishwa na tathmini iliyofanywa na Kampuni ya Moodys mwezi Machi 2025 ambapo Tanzania ilibakizwa katika daraja B1 ikiwa na mwelekeo imara matarajio haya yanaweza kuathiriwa na vikwazo vya kibiashara na migogoro ya kisiasa duniani kwa mwenendo wa uchumi pamoja na matarajio yake ni katika robo ya kwanza ya mwaka 2025, hali ya ukwasi illimarika, kutokana na ongezeko la matumizi ya Serikali pamoja na kupungua kwa fedha taslimu nje ya mfumo wa benki na kutokana na mwenendo huu, benki zilipunguza mahitaji ya mikopo kutoka Benki Kuu.
Ameongeza kamati ilibaini kuwa baadhi ya benki ndogo zimeendelea kukumbana na changamoto ya kupata ukwasi kwa gharama nafuu na hivyo kuchangia riba ya mikopo ya siku saba baina ya benki kubaki karibu ya wigo wa juu wa riba ya Benki Kuu (CBR).
Amesema kwa mwaka 2024, uchumi wa Tanzania ulikuwa imara, ukichangiwa na ongezeko la uwekezaji katika sekta za umma na binafsi na ukuaji wa uchumi kwa Tanzania Bara unakadiriwa kufikia asilimia 5.5 mwaka 2024, ukilinganishwa na matarajio ya ukuaji wa asilimia 5.4, na ukuaji wa asilimia 5.1 mwaka 2023.
Amesema ukuaji huo ulichangiwa zaidi na sekta ya kilimo, fedha na bima, uchimbaji wa madini, na ujenzi. Vilevile, utalii ambao hugusa shughuli nyingi za kiuchumi ulichangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa uchumi.
Amesema deni la Serikali limeendelea kuwa himilivu, hali inayoakisi usimamizi thabiti wa mapato na matumizi ya Serikali na sekta ya nje imeendelea kuimarika. Katika mwaka unaoishia Machi 2025, nakisi ya urari wa malipo ya kawaida ilikuwa takriban asilimia 2.6 ya Pato la Taifa ukilinganishwa na asilimia 3.7 kwa kipindi kama hicho mwaka 2024, kutokana na ongezeko la mauzo nje ya nchi hususan utalii, dhahabu, korosho na tumbaku.
Amesema kwa upande wa Zanzibar urari wa malipo ya kawaida ulikuwa ziada ya dola milioni 563.5 ikilinganishwa na ziada ya dola milioni 407.4 kwa mwaka ulioishia mwezi Machi mwaka 2024, kutokana na ongezeko la mapato ya utalii.
Vilevile amesema akiba ya fedha za kigeni iliendelea kuwa ya kutosha katika robo ya kwanza ya mwaka 2025 na akiba ya fedha za kigeni ilifikia zaidi ya dola bilioni 5.6 kiasi kinachotosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi kwa takribani miezi 4.5, na inatarajiwa kubaki katika viwango hivi kwa robo ya pili ya mwaka 2025.
“Kulingana na matarajio ya kuimarika kwa urari wa malipo ya kawaida, Kamati ilibaini kuwa mabadiliko ya thamani ya shilingi katika robo ya kwanza ya 2025 ni ya msimu, na hivyo Shilingi inatarajiwa kuimarika sambamba na ongezeko la mapato ya fedha za kigeni nchini,“amesema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA), Theobald Sabi ni ishara nzuri ya kuendelea kuwa kwenye kiwango hicho na aliipongeza benki kuu kwa hatua walizochukua mwaka jana na kuendelea kuhakikisha uchumi unakuwa imara.



