Na Mwandishi Wetu,Dodoma
MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajia kuchukua fomu ya kugombea urais kesho, Agosti 9, 2025, katika ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), zilizopo Njedengwa, Dodoma.

Hayo yamebainishwa mapema leo Agosti 8,2025 na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla, wakati akizugumza na waandishi wa habari ambapo amesema fomu hiyo atachukua saa 10:50 asubuhi, sambamba na mgombea mwenza, Dkt. Emmanuel Nchimbi.
Makalla amesema Tume ya Uchaguzi imetoa ratiba rasmi ya uchaguzi ambayo inaonyesha uchukuaji wa fomu za urais utaanza Agosti 9 hadi 27, wakati ubunge na udiwani ni kuanzia Agosti 14 hadi 27. Uchaguzi Mkuu utafanyika Oktoba 28, 2025.
“Kwa upande wa CCM, mchakato wa ndani wa kupata wagombea ulishakamilika mapema Januari mwaka huu. Kwa hiyo Dkt. Samia kama mgombea wa CCM atachukua fomu rasmi kesho,” amesema Makalla.
Baada ya kuchukua fomu, Dkt. Samia atakwenda Makao Makuu ya CCM Dodoma kusaini kitabu cha wageni na kusalimiana na wananchi na wanachama wa CCM waliokaribishwa kuhudhuria tukio hilo.
Makalla amesema baada ya hatua hiyo, chama kitaendelea na mchakato wa ndani ikiwemo uteuzi wa wagombea wa ubunge na udiwani, kabla ya kuanza rasmi kampeni kuelekea uchaguzi mkuu.



