Home KITAIFA TSB imewataka Wananchi na wawekezaji kuchangamkia fursa za zao la mkonge

TSB imewataka Wananchi na wawekezaji kuchangamkia fursa za zao la mkonge

Na Esther Mnyika, Dar es Salaam

BODI ya Mkonge Tanzania (TSB) imewataka Wananchi na wawekezaji kuchangamkia fursa zinazotokana na zao la mkonge baada ya kuongezeka kwa mahitaji ya mbegu, mitambo ya usindikaji na bidhaa zinazotokana na zao hilo.

Akizungumza Agosti, 7,2025 kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo Nanenane jijini Dodoma, Mkuu wa Sehemu ya Maendeleo kutoka TSB, Simon Kibasa amesema sekta hiyo kwa sasa imepiga hatua kubwa kibiashara na kuibua mahitaji makubwa sokoni.

Amesema uzalishaji wa mkonge umeongezeka kutoka tani 39,000 mwaka 2020 hadi tani 61,000 mwaka 2024, huku idadi ya wakulima ikiongezeka kutoka 7,551 hadi 20,000 katika kipindi hicho.

“Kwa sasa, mahitaji ya mbegu za mkonge kitaifa ni zaidi ya milioni 60, wakati uzalishaji uliopo ni chini ya milioni 25. Hii inamaanisha kuna pengo la mbegu milioni 35, ambalo linaweza kuzibwa na wawekezaji wapya,” amesema Kibasa.

Kibasa amebainisha kuwa pamoja na uwekezaji wa serikali kwenye mitambo ya usindikaji, bado kuna uhitaji wa zaidi ya mitambo mikubwa 25 ya kusimika mkonge. Aidha, alitaja fursa nyingine kuwa ni biashara ya kuuza singa za mkonge ndani na nje ya nchi, pamoja na kuongeza thamani kwa kutengeneza bidhaa kama vikapu, kamba na magunia.

“Tasnia ya mkonge iliporomoka kati ya mwaka 1984 hadi 2011 kutokana na ushindani wa bidhaa za plastiki, lakini sasa inapata uhai mpya kutokana na ongezeko la mahitaji ya bidhaa rafiki kwa mazingira, ikiwemo vifaa vya magari kama dashboard,” ameongeza.

Ametaja pia ubunifu mwingine katika sekta hiyo kuwa ni kuzalisha uyoga kwa kutumia mabaki ya mkonge baada ya usindikaji, akisema soko la uyoga ni kubwa na lenye faida.

Bodi ya Mkonge Tanzania, iliyo chini ya Wizara ya Kilimo, inasimamia maendeleo ya zao hilo na inashiriki Nanenane ili kutoa elimu kwa wananchi kuhusu fursa zilizopo katika kilimo, biashara na teknolojia ya mkonge.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here