Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
BENKI ya CRDB imetenga kiasi cha shilingi bilioni 171.83 zilizopatikana kupitia mauzo ya hatifungani za kijani (green bond) kwaajili ya kutoa mikopo itakayosaidia wananchi kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi.

Akizungumza leo Septemba,9 2025 katika hafla ya uzinduzi wa mikopo hiyo jijini Dar es Salaam, Afisa Mkuu wa Biashara wa CRDB, Boma Labala, amesema mikopo hiyo itaelekezwa kwa wadau katika sekta ya nishati, hasa ya kupikia, nishati jadidifu, urejelezaji wa taka, pamoja na kilimo cha kisasa kinachojali mazingira.
Labala amesema kuwa mikopo hiyo ni hatua muhimu katika kuunga mkono juhudi za Tanzania za kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi na kuboresha mazingira.
“Lengo letu ni kuhakikisha kwamba sekta za nishati, kilimo, na mazingira zinapata msaada wa kifedha ili kutekeleza miradi ya kijani na endelevu,” amesema Labala.
Aidha ameeleza kuwa mikopo hiyo itakuwa na riba nafuu na masharti nafuu kwa wadau wa nishati ya kijani, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza matumizi ya nishati safi na kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa jamii. Alisema kuwa CRDB itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha kuwa miradi ya kijani inafaidi jamii na uchumi wa taifa.

Kwa upande mwingine, Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la Kimataifa la Uwezeshaji Mitaji (IFC), Martine Valcin, alisema kuwa Tanzania inahitaji zaidi ya dola bilioni 19 ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi.
Ameongeza kuwa mikopo hii ni muhimu kwa kuwezesha nchi kufikia malengo yake ya kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa na kuongeza matumizi ya nishati mbadala.
Naye Mkurugenzi wa Power Safe, Paul Koyi, ameeleza kuwa mikopo hiyo itasaidia watu wengi kumudu ununuzi wa vifaa vya nishati mbadala kama vile mifumo ya nishati ya jua na biogas, hivyo kuboresha upatikanaji wa nishati safi na endelevu.
Amefafanua kuwa utekelezaji wa mikopo hiyo itatoa manufaa makubwa kwa jamii, ikiwemo kuboresha hali ya maisha na kupunguza utegemezi wa nishati hatarishi kwa mazingira.
Pia, ameongeza kuwa programu hiyo inalenga kutoa fursa kwa wajasiriamali wadogo na mashirika madogo ambayo yanashughulika na miradi ya nishati mbadala, kama vile paneli za jua na mifumo ya umeme wa wind, kuwawezesha kutekeleza miradi ya kijani.
“Hii itasaidia kuhamasisha matumizi ya teknolojia zinazohifadhi mazingira, na hivyo kuchangia katika kupambana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi,” amesema Koyi.
Uwekezaji huo wa CRDB ni hatua muhimu katika kuunga mkono juhudi za Tanzania za kutekeleza mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi Benki hiyo inatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kuboresha mazingira, kuwezesha wananchi na kuendeleza sekta endelevu zinazozingatia mazingira



