Dar es Salaam
MSAJILI wa Vyama Vya Siasa, Jaji Francis Mutungi amewataka viongozi wa vyama vya siasa kuwahimiza wananchi wakiwemo wanachama wao, kufuata sheria kudumisha amani na mshikamo hususan kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu.

Jaji Mutungi ameyasema hayo Mei, 3 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa kikao maalumu na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari kujadili masuala tofauti ikiwemo maandalizi ya uchaguzi.
“Ni vyema tukawa makini kipindi hiki hususan viongozi wa vyama vya siasa, wajue kuwa uchaguzi utapita maisha yataendelea, tudumishe amani na mshikano kwani ndiyo msingi wa maendeleo,”amesema.
Amesema kuelekea katika Uchaguzi Mkuu ambacho huwa kinakuwa na matukio mengi na ongezeko la joto la uchaguzi katika nchi zote, ni vyema kuwa makini kuhakikisha kuwa demokrasia inadumishwa.

“Katika kipindi kama hiki, habari za uongo huwa zinaongezeka, yaani habari zisizo na vyanzo halisi, mfano ni ule waraka wa TEC, ulioghushiwa, ni vyema wananchi wakatafuta taarifa katika vyanzo rasmi vinavyoaminika,”amesema.
Amesema kwasasa wameanza utaratibu wa kuvijengea uwezo vyama vya siasa katika masuala ya uchaguzi mkuu, ambapo walianza Zanzibar na wataendelea Dar es Salaam, lengo ikiwa ni kuhakikisha kuwa vyama vinapata maarifa ya kutosha kushiriki uchaguzi kwa amani na mshikamano.
Amesema wataendelea kushirikiana na vyombo vya habari na watatoa mafunzo kuelekea uchaguzi mkuu kuwajengea uwezo kwa namna njema ya kutekeleza majukumu yao.

Jaji Francis amesema wanaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa uchaguzi ikiwemo Tume Huru ya Uchaguzi na ile ya Zanzibar, kuhakikisha wanazingatia maadili na kudumisha aman Alivitaka vyombo vya habari kuhakikisha vinaripoti taarifa zenye usahihi kwani vina nafasi kubwa katika kulinda amani ya nchi na kufanikisha uchaguzi huru, haki na amani.
Kuhusu mchango wa vyombo vya habari, amesema vina umuhimu mkubwa kujenga jamii yenye amani, kwa kuandika habari sahihi za haki ambazo haziegemei upande wowote.

“Katika hilo, tunaandaa mafunzo kwa vyombo vya habari, kuvielimisha msingi wa kanuni na sheria tunazozisimamia katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu kuhakikisha unakuwa wa demokrasia,”amesema.
Amesema watahakikisha uchaguzi, unatoa nafasi sawa kwa washiriki wote wanawake na wanaume, kujenga haki sawa kwa wote.
Amesisitiza kuwa, vyombo vya habari ni daraja la kuelimisha jamii, kuhoji na kutoa fursa kwa washiriki wa uchaguzi kueleza sera zao, hivyo watashirikiana na vyombo vya habari kwa ukweli na uwazi kufanikisha lengo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Deodatus Balile, amesema wamefurahi kushiriki katika mkutano huo na msajili wa vyama vya siasa, huku akivitaka vyombo vya habari na wananchi kuwa makini kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu kwani matumizi ya akili mnemba yanakuwa makubwa kwa lengo la kuchafuana na kupotosha.

Amevitaka vyombo vya habari kuwa makini na kuhakikisha kuwa wanachapisha habari zenye vyanzo halisi vya kweli kuepuka upotoshaji unaoweza kufanywa kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu.