📌 REA yapata kibali kufunga miundombinu ya nishati safi ya kupikia katika Shule 115
Dodoma
NAIBU Waziri Nishati, Judith Kapinga amesema hadi kufikia mwezi Machi 2025 takribani Shule za Serikali 216 zimehamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia ambapo kati ya hizo, Sekondari 146 zinatumia gesi ya LPG.

Kapinga ameyasema hayo leo Mei 7, 2025 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la la Mbunge wa Liwale, Zuberi Mohamedi Kuachauka aliyeuliza ni lini majiko yanayotumia gesi yataanza kutumika kote nchini.
“Serikali kupitia REA inaendelea kutoa ruzuku ya ujenzi wa miundombinu ya nishati safi ya kupikia kwa shule nyingine na tarehe 20 Aprili, 2025, REA kupitia Wizara ya Nishati imepokea kibali kutoka TAMISEMI cha kufunga miundombinu ya huduma ya nishati safi ya kupikia katika shule 115 zikiwemo shule za Mikoa za sayansi za wasichana 16; shule za kitaifa za wavulana 7, shule za bweni za kawaida 66 na shule kongwe za sekondari 26,”amesema Kapinga.
Amesisitiza kuwa Serikali kupitia REA na wadau mbalimbali itaendelea kufunga miundombinu ya nishati ya kupikia katika shule za sekondari kulingana na upatikanaji wa fedha.
Kapinga ameongeza kuwa Wizara ya Nishati kupitia Wakala wa Nishati Vijijini i(REA) inatekeleza miradi ya kufunga mifumo ya nishati safi ya kupikia Jeshi la polisi na Magereza katika Mikoa 24, jeshi la Zima Moto pamoja na huduma za Wakimbizi.
Aidha, amesisitiza kuwa upo mkakati wa kufunga mifumo ya nishati safi ya kupikia katika Taasisi zilizo chini ya Wizara ya afya ikiwemo hospitali za Mikoa, za Wilaya na za kitaifa takribani 21.
Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Tunza Malapo aliyetaka kufahamu ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha shule, Zahanati na Vituo vya afya vipya vinajengwa vikiwa na mifumo ya nishati safi ya kupikia, Kapinga amesema kupitia mkakati wa nishati safi ya kupikia ambao utekelezaji wake umeanza kutekelezwa, Serikali inaelekea kwenye mtazamo huo wa Shule, Zahanati na Vituo vya afya kujengwa sambamba na miundombinu ya nishati safi ya kupikia.