Dar es Salaam
SERIKALI ya Tanzania na Msumbiji zimesaini mikataba miwili pamoja na hati nne za makubalino ya uhusiano katika sekta mbalimbali zikiwemo elimu,uchukuzi pamoja na utamaduni.

Mikataba na hati hizo zimesainiwa na mawaziri wa nchi hizo mbili mbele ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Msumbiji Daniel Francisco Chapo Ikulu jijini Dar es Salaam.
Akizungumza leo Mei, 8 2025 Jijini Dar es Salaam baada yakusaini mikataba na hati hizo za makubaliano Rais Dk.Samia amesema hatua hiyo ni muendelezo wa ushirikiano baina ya nchi hizo mbili ambazo zimekuwa karibu tangu wakati wa Ukombozi wa nchi hizo.

“Miongoni mwa sehemu ambazo tutashirikiana ni kuimarisha uhusiano yakibiashara na uwekezaji,licha ya ujirani tulionao lakini ushirikiano wetu wa kiuchumi bado haujaenda sambamba na ukaribu tulioonao,”amesema Dk.Samia.
Amesema ushirikiano huo pia unalenga kusaidia wafanyabiashara ambapo kutaanzishwa kituo cha pamoja mpaka mwa Tanzania na Msumbiji kwa ajili yakuwarahisishia wafanyabiashara.

“Kwa sasa watu wanafanya biashara katika maeneo tofauti ambayo yanapatikana na nchi hizi mbili lakini kupitia makubaliano haya tutakuwa na kituo cha pamoja pale Mtambaswala Mtwara ambapo ni mpakani mwa Tanzania na Msumbiji lengo letu tuinuke pamoja kiuchumi,”amesema Dk.Samia.
Amesema mambo mengine waliyokubaliana ni ujenzi wa barabara ambazo zitaunganisha nchi hizo mbili,ushirikiano katika masuala ya anga pamoja na usafiri wa majini kupitia Ziwa Nyasa.

“Pia nimemueleza kuhusu miradi yakimkakati kama mradi wa Treni ya Mwendokasi (SGR) ambapo atatembelea kwa sababu tuna mpango wakuanzisha safari za SGR Msumbiji,”amesema.
Amesema pia wamezungumzia ushirikiano kuhusu matumizi ya rasilimali ya bahari ambapi atatembelea Mamlaka ya Usimamizi wa Pamoja wa Bahari iliyopo Zanzibar pamoja na kutembelea soko la samaki lililopo Malindi.

“Mambo mengine tuliyokubaliana kushirikiana ni katika masuala ya mawasiliano,madini elimu,afya,amani na usalama pamoja na utengano wa bara la Afrika,”amesem.
Amesema amekutana Rais Chapo ambaye ni ziara yake ya kwanza tangu aapishwe siku 100 zilizopita lengo la mazungumzo hayo ni kuimarisha mahusiano.
Akizungumza Rais wa Msumbiji, Chapo amesema ziara hiyo inalenga kukuza mahusiano yakindugu,kirafiki na kihistoria.

“Tumekuwa na mazungumzo kabla ya mkutano huu kuhusu maeneo yakubadilisha mawazo katika masuala yakiuchumi,biashara pamoja na kukuza mahusiano yakisiasa ambayo teyari tunayo mazuri na ya kiusalama,”amesema Chapo.
Amesema pia majadiliano na makubaliano hayo pia yana lengo la kuunganisha majiji ya Dar es Salaam iliyopo Tanzania pamoja na jiji la Pemba na Maputo yaliyopo Msumbiji.
Amesema wanataka kukuza ushirikiano katika masuala ya biashara ya bahari ,usalama wa bahari,usafiri wa anga kati ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) pamoja na Msumbiji.
Amesema ushirikiano huo pia utahusisha kuanzisha eneo la ushirikiano katika maeneo mapya ya uchumi wa buluu.
“Nchi zetu zinazungukwa na bahari kwa hiyo tuna utajiri mkubwa sana wa bahari hivyo tunapaswa kuungana ili uweze kutunufaisha,”amesema Chapo.
Mikataba iliyosainiwa ni pamoja uanzishwaji wa kituo Kimoja cha Forodha,mkataba wakubadilishana wafungwa kati ya Tanzania na Msumbiji.
Pia walisaini hati nne za makubaliano ikiwemo kubadilishana wanafunzi wa programu mbalimbali kati ya Tanzania na Msumbiji,makubaliano yakushirikiana katika masuala ya utamaduni,ushirikiano baina ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na redio ya Msumbiji pamoja ushirikiano wa Mamlaka ya Vifaa Tiba Tanzania (TMDA) pamoja na Mamlaka ya Taifa ya Kudhibiti Madawa Msumbiji.