Home KITAIFA DINI ZINA MCHANGO MKUBWA KATIKA KUIMARISHA USTAWI WA JAMII

DINI ZINA MCHANGO MKUBWA KATIKA KUIMARISHA USTAWI WA JAMII

Dar es Salaam

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema madhehebu ya dini yana mchango mkubwa katika kuimarisha ustawi wa jamii na kutoa huduma za kiroho.

Amesema kwa kutambua hilo, Dk. Samia Suluhu Hassan wakati wote amekuwa akitekeleza kwa vitendo dhamira ya kukuza ushirikiano kati ya Serikali na madhehebu ya dini.

Amesema hayo leo Mei 10, 2025 alipomuwakilisha Dk. Samia katika kilele cha dua maalum ya kuombea viongozi wa Kitaifa, amani, uchaguzi mkuu pamoja na kuwaombea mamufti na masheikh waliotangulia mbele za haki, kwenye Viwanja vya Msikiti wa Mohammed VI, Kinondoni Dar es Salaam.

“Ni ukweli usiopingika sote tumeshuhudia kuwa Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jinsi gani anawathamini, anawasilikiza na kuwashirikisha viongozi wa madhehebu ya dini katika masuala muhimu ya kitaifa,”amesema.

Majaliwa amempongeza Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Sheikh Dkt. Abubakar Zubeir bin Ali Mbwana kwa kuandaa dua hiyo kwa ajili ya baraka na amani ya Tanzania wakati wa uchaguzi mkuu.

“Nikiri kwamba Serikali inatambua umuhimu wa sala na dua. Viongozi tunatekeleza majukumu yetu kwa salama kwa kuwa viongozi wetu wa dini na waumini wote mnatuombea dua. Hii ndiyo sababu Serikali imekuwa ikishirikiana na madhehebu ya dini katika shughuli zake,”amesema.

Ameongeza kuwa Serikali inathamini kazi kubwa inayofanywa katika maeneo mbalimbali hususan katika kutoa huduma za kijamii na hivyo kuchangia kasi ya maendeleo ya Taifa letu. “Huduma hizo ni pamoja na zile za elimu, afya, maji, nishati, mafunzo kuhusu kilimo bora na ufugaji, na huduma nyingine mbalimbali.”

Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya dua hiyo Kitaifa Hajati Mwamtumu Mahiza amesema kuwa dua hiyo ni kwa ajili ya kuwaombea masheikh na Mamufti walioleta mchango chanya katika dini ya kiislamu.

Amesema kuwa dua hiyo ambayo imefanyika kwa siku tatu ililenga kuombea viongozi wakuu wa nchi na wote wanaoingia kwenye mchakato wa uchaguzi pamoja na kuombea amani nchini.

“Tunahitaji kuwa wanyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu kwa sababu anasema katika Quran kuwa niombeni nami nitawapa, tunataka kuingia kwenye uchaguzi mkuu na kutoka tukiwa salama na wamoja,”amesema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here