Na Esther Mnyika, Kilimanjaro
RAIS Dk.Samia Suluhu Hassan kesho anatarajia kuongoza Watanzania mazishi ya aliyekuwa Makamu wa Rais wa Kwanza na Waziri Makuu wa zamani, Hayati Cleopa David Msuya.

Msuya alifariki Mei, 7 2025 Hospitali ya Mzena mkoani Dar es Salaam alipokua akipatiwa matibabu ya moyo yaliyokuwa yakimsumbua na kutibiwa katika Hospitali kadhaa ikiwemo Hospitali ya Taifa Muhimbili- Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete(JKCI), kilichopo jijini Dar es Salaam na nchi za nje.
Hayati Msuya alizaliwa Januari 4,1931 katika Kijiji cha Chomvu, Usangi, Wilayani Mwanga, mkoani Kilimanjaro ambapo mazishi pia yatafanyika mkoani humo.
Leo Mei, 12 2025 wananchi wa Wilaya ya Mwanga na maeneo ya jirani walipata nafasi ya kutoa salamu za mwisho kwa mwili wa Hayati Msuya katika viwanja vya Cleopa Msuya vilivyopo wilayani Mwanga wakiongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya WaziriMkuu(Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi.

Akizungumza kwa niaba ya Mawaziri Wakuu Wastaafu, Waziri Makuu Mstaafu Mizengo Pinda alisema Hayati Msuya alifanya kazi serikalini Kwa muda mrefu na kuacha mambo mengi mazuri.
Pinda ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa 10 wa Tanzania akipokea nafasi hiyo kutoka kwa Edward Lowassa na kufuatiwa na Kassim Majaliwa.
Amesema miongoni mwa mambo aliyokuwa akiyapenda kutoka kwa Hayati Msuya ni ukweli wake hata katika mazingira magumu.
Amesema kutokana na hali hiyo,alikua akienda kukutana naye ili kupata busara za kusemwa kwa Watanzania.
“Yeye anajua kwani Mwanga Mimi nina upenzi wa aina yake, na ndiyo maana nikapima niende wapi, najua yapi mambo yalitokea na kupitia Mzee huyu yamefanikiwa,”amesema.

Ametoa wito kwa wananchi kutowachagua viongozi wanaotoa fedha na nguo kuelekea Uchaguzi Makuu kwa wanaotaka nafasi za Ubunge na nafasi zingine za uwakilishi.
Amesisitiza viongozi wa dini kuliombea Taifa ili Mungu azidi kuibafiki nchi , kushikamana na kuungana.
Naye Askofu mteule wa dayosisi ya Mwanga, Dk. Daniel Mono amewataka wananchi waliohudhuria kuaga mwili wa Hayati Msuya, alikua akilioenda kanisa, mwalimu wa wengi aliyeliyelinda Imani.

“Siwezi kuwa na maneno ya kutosha kwa mtu huyu, hakuwa mbinafsi tuendeleze yale yote aliyoyatenda, siku hizi tukipata cheo kidogo hata kanisani kwa ‘appointment’ alikuwa mnyenyekevu mbele ya kanisa.
Alifanya maendeleo kwa wanamwanga na alihimiza kufanya kazi. Alihimiza kuwa wamoja wasibaguane kwaajili ya dini, tumshukuru Mungu kwaajili ya maisha yake,”amesema.
Ametoa wito kwa kila anaetaka kuwa Kiongozi aweke maslahi ya wananchi mbele wanamwanga tusibaguane kwa sababu ya dini tuihi kwa umoja.

“Tujifunze kwa Cleopa alikuwa akimtumikia Mungu pamoja na kuwa na nyadhifa mbalimbali Serikalini,”amesema.
Amewaonya Watanzania kuelekea Uchaguzi Mkuu kukataa wagombea wanaonunua wanachama na kwamba wawachague wenye sifa.
Awali akitoa salamu za rambirambi, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema Hayati Msuya alitoa mchango mkubwa na Maendeleo katika Jimbo hilo kwakua alikua Mbunge kwa miaka ipatayo 20.
Amesema kutokana na hayo, watamkumbuka kwa mengi aliyoyafanya katika Mkoa huo ambao umepiga hatua kubwa ya Maendeleo katika Wilaya hiyo ikiwemo Barabara za lami, elimu, upatikanaji wa umeme na maji.
Amesema Hayati Msuya alikua kiongozi mwenye upendo, ushirikiano kwa rika zote, mnyenyekevu asiyekua na majivuno aliyewashauri na kuwaasa juu ya mambo mengi ya maendeleo.
Amesema Hayati Msuya alikua hasahau jambo na aliyetaka utekelezaji kwa kufuatilia ambapo siku za mwisho za uhai wake alikua kinara wa kumuomba Rais, Dk. Samia kukamilisha mradi wa maji wa Same- Mwanga -Korogwe ambao ulikamilishwa na kushiriki kikamilifu Uzinduzi wa mradi huo.

Mradi wa Same-Mwanga-Korogwe ulizinduliwa Machi 9,2025 na Rais Dk. Samia utakaowahakikishia wananchi wa miji ya Same, Mwanga na vijiji 38 vya wilaya za Same, Mwanga na Korogwe huduma ya uhakika ya majisafi na salama.
Mradi huo ambao aliuweka jiwe la msingi Novemba 12, 2018 akiwa Makamu wa Rais, kukamilika kwake Kwa awamu ya Kwanza kumeongeza upatikanaji wa maji kutoka Lita Milioni 3.7 Kwa siku hadi Lita Milioni 51.7 Kwa siku hatua ambavyo imeleta ahueni kwa wananchi wa Wilaya ya Same, Mwanga na Korogwe.
“Hakika mchango wa Msuya umeacha alama kubwa katika Maendeleo ya Mkoa wa Kilimanjaro na Taifa kwa ujumla na hatutamsahau tutayatimiza yote aliyokuwa akiyaeleza ,”amesema.
Akizungumza kwa niaba ya wabunge, Mbunge wa Jimbo la Mwanga, Anania Tadayo amesema wamehuzunishwa na hakuna mchoko wa maono yake na kuwasisitiza kujianini katika kutenda kazi na kusisitiza umoja.
Amesema wanapaswa kutotikisika na kwamba waendeleze Yale yote waliyoyapata kwa Hayati Msuya.