Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imepanga kutekeleza vipaumbele vitano muhimu katika bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026, ikiwa ni mkakati wa kuboresha upatikanaji na ubora wa elimu nchini.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo leo Mei 12, 2025 bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, alisema vipaumbele hivyo ni pamoja na kuendelea kutekeleza sera na mitaala ya elimu, kufanya mapitio ya sheria pamoja na kuandaa miongozo ya utoaji wa elimu na mafunzo.
Vipaumbele vingine ni kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya awali, msingi, sekondari na ualimu; pamoja na elimu ya juu na utafiti, hususan katika matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu ili kuchangia maendeleo endelevu ya taifa.
Kadhalika, Serikali itaendelea kuimarisha elimu ya amali katika shule za sekondari na vyuo vya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi ili kuongeza ujuzi kwa vijana.
Profesa Mkenda alibainisha pia kuwa juhudi zaidi zitaelekezwa katika kuwasomesha vijana wa Kitanzania nje ya nchi kwenye maeneo ya sayansi ya nyuklia, kompyuta na akili bandia ili kuongeza wataalam wa teknolojia ya kisasa.