Home KITAIFA Dk. Mwinyi aeleza majuto yake kwa Charles Hilary, atoa wito kwa waajiri

Dk. Mwinyi aeleza majuto yake kwa Charles Hilary, atoa wito kwa waajiri

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameeleza kwa masikitiko majuto yake ya kutomweleza mapema marehemu Charles Hilary jinsi alivyomthamini na kuvutiwa na weledi wake kazini, akimtaja kuwa mchapakazi, mcheshi, na mzalendo aliyehudumu kwa uadilifu mkubwa katika taasisi mbalimbali za habari ndani na nje ya nchi.

Akizungumza leo, Jumatano Mei 14, 2025, katika viwanja vya Mapinduzi Square wakati wa hafla ya kuuaga mwili wa marehemu Charles Hilary, Dk. Mwinyi ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa waajiri nchini kuwatambua na kuwasifu wafanyakazi wao wanapofanya vizuri badala ya kusubiri hadi kufariki kwao.

“Ndugu zangu katika msiba huu kuna fundisho tunalipata. Fundisho lenyewe ni kwamba tuwe tayari kuwasifu na kuwaambia wafanyakazi wetu wakifanya vema palepale wanapofanya vema. Tusingoje mpaka mtu kashatangulia mbele ya haki, ndiyo tutoe sifa zake,” amesema Dk. Mwinyi kwa uchungu.

Ameeleza kuwa ni jambo la majuto kwake kutomwambia marehemu Charles mapema maneno ya shukrani aliyoyahifadhi moyoni mwake hadi kifo kilipowatenganisha.

“Kama kuna jambo ninalolijutia, ni kutomwambia Charles mapema. Tumeondokewa na mtu mzuri, mtu mchapakazi, mtu hodari wa kazi yake. Lakini hii ni mapenzi ya Mungu, na sote tupo katika njia hiyo,” alisema kwa sauti ya huzuni.

Ahadi kwa familia ya Charles

Katika hotuba yake, Dk Mwinyi amefichua pia kuwa Charles alimpa ombi binafsi linalohusu familia yake ambalo atalitimiza kwa heshima ya kazi nzuri aliyomfanyia.

“Sikupata nafasi ya kukutana na mke wake wala watoto wake lakini nilikuwa nawajua sababu alikuwa ananizungumzia kuhusu wao. Naomba nisiseme hapa lakini alinipa ombi linalohusiana na familia yake… nitalitimiza. Nitaenzi kazi aliyonifanyia kwa kutimiza yale ambayo aliyataka juu ya familia yake,” ameahidi Dk Mwinyi.

Ucheshi na ukaribu wa Charles

Akielezea tabia ya Charles, Dk Mwinyi amesema alikuwa mtu mwenye ucheshi wa kipekee aliyeweza kupunguza msongo wa mawazo hata katika mazingira ya kazi yenye presha kubwa.

“Na mimi nayathibitisha haya, sababu mara zote tulipokuwa naye hata kama una ‘stress’ kiasi gani utacheka tu. Alikuwa hodari, na mtu mcheshi wa kutufanya sote tu-‘relax’ pamoja na majukumu. Kwa ofisi yangu mimi ambayo ina mambo mengi, stress ni kawaida, lakini mbele ya marehemu Charles tulikuwa tunacheka, tunafurahi,” amesema kwa kutabasamu.

Ameeleza zaidi kuwa marehemu alihudumu katika taasisi nyeti za habari kama RTD (sasa TBC), Radio One, AZAM TV, BBC, DW (Ujerumani) kabla ya kuitwa kujiunga Ikulu ya Zanzibar.

Safari ya kujiunga na Ikulu

Dk Mwinyi pia amesimulia namna alivyomwita Charles kujiunga naye kama Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais- Ikulu Zanzibar, akimtaja kuwa hakusita wala kuomba muda wa kufikiria.

“Nilimwambia kidiplomasia kidogo; chukua muda, tafakari halafu unijibu. Lakini akaniambia, ‘kwa heshima uliyonipa nakujibu sasa hivi kwamba niko tayari kuchukua kazi hiyo kuja kufanya kazi na wewe’. Namshukuru sana marehemu kwa moyo wake wa kizalendo,” amesema.

Ameongeza kuwa baada ya kuafikiana na Charles, alimpigia simu Abubakary Bakharesa, mmiliki wa AZAM TV, ili kumwomba amruhusu kujiunga na serikali, naye pia hakusita.

“Nikamuomba kwa heshima, na yeye akaniambia: ‘madamu unamhitaji, na sisi tunamhitaji lakini tuko tayari kukupa-tunatambua kazi unayompa ni ya nchi’.”

Charles Hilary alifariki dunia Mei 11, 2025, jijini Dar es Salaam baada ya kuugua kwa muda mfupi. Mwili wake umesafirishwa visiwani Zanzibar ambapo maziko yanatarajiwa kufanyika leo saa 10:00 jioni katika makaburi ya Mwanakwerekwe, mara baada ya shughuli ya kuaga kumalizika.

Msemaji wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Gerson Msigwa, akizungumza kwa niaba ya Serikali ya Muungano, alisema Charles alikuwa mfano wa kuigwa katika utendaji kazi, mtu ambayehakuwa na mipaka ya majukumu kwa kuzingatia umri wala nafasi aliyonayo kazini.

“Alikuwa tayari kufanya kazi wakati wowote, bila kujali ukubwa wa jina au nafasi yake. Tutamkumbuka kwa bidii, weledi na moyo wa kujitolea kwa Taifa,” ameema Msigwa.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Fatma Hamad, ameeleza kuwa Charles alikuwa kati ya watu waliokuwa mstari wa mbele kuhamasisha matumizi ya lugha ya Kiswahili ndani na nje ya Tanzania, hivyo alihusika kikamilifu kuipeperusha bendera ya Taifa kupitia lugha hiyo.

Kwa upande wake, Msaidizi wa Mawasiliano ya Rais – Ikulu Zanzibar, Rakiy, alieleza kuwa ofisi hiyo imepoteza mtu muhimu mno, akisisitiza kuwa Charles alikuwa na umahiri wa hali ya juu na aliwajali watu aliokuwa nao kazini.

“Charles alikuwa mcheshi sana akiwa nje ya kazi, na alitufundisha kupendana na kuacha tabia ya kuweka mambo rohoni. Katika kipindi hiki kigumu ametufundisha kuwa na subira na mshikamano,” alisema Rakiy.

Salamu maalum kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, zilisomwa na Mshauri wa Siasa wa Rais, ambaye aliwasilisha nyongeza ya pole kwa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, akieleza kuwa Charles hakuwa tu msaidizi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar bali pia rafiki na mshirika wa karibu wa viongozi wote wa kitaifa.

“Nyongeza hii ya pole inakwenda moja kwa moja kwa Dk Mwinyi kwa sababu huu ni msiba wake pia. Jana walikuwa pamoja, leo wanamwaga machozi. Kwa kweli Taifa limepoteza mtu wa kipekee,” alisema mshauri huyo.

Aliongeza kuwa viongozi na wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) watamkumbuka Charles kwa namna alivyokuwa akisemea kwa umahiri utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, huku akieleza mafanikio ya Serikali kwa ufasaha mkubwa uliogusa mioyo ya wananchi.

Mazishi ya Charles Hilary yanatarajiwa kufanyika leo saa 10 jioni katika makaburi ya Mwanakwerekwe, Zanzibar, ambapo familia, marafiki, viongozi na wananchi wa kada mbalimbali wanamzika mpendwa wao kwa heshima ya kitaifa.

Charles ameacha historia ya kuwa miongoni mwa watumishi wachache wa umma waliotumikia vyombo vikuu vya habari vya kitaifa na kimataifa kwa ufanisi, akihitimisha safari yake ya utumishi kama msemaji mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mapema akisoma wasifu wa baba yake, Faidha Hilary, amesema Charles Martine Hilary alizaliwa Oktoba 22, 1959 Mtaa wa Jang’ombe visiwani Zanzibar.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here