Home SIASA Gavu asisitiza kuimarisha ushirikiano Tanzania, China

Gavu asisitiza kuimarisha ushirikiano Tanzania, China

China

KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Idara ya Oganaizesheni, Issa Gavu, amesisitiza umuhimu wa kuendeleza uhusiano baina ya Tanzania na Jamhuri ya Watu wa China kwa maslahi ya nchi hizo na watu wake.

Pia, amehimiza kudumisha uhusiano wa karibu kati ya CCM na Chama Cha Kikomunisti cha China (CPC).

Gavu ameeleza hayo leo Mei, 15 2025 katika hafla ya
uzinduzi wa mafunzo maalum ya kuimarisha ushirikiano wa kihistoria kati ya Tanzania na China, pamoja na kudumisha uhusiano wa kati ya CCM na CPC, yanayofanyika katika Chuo cha Shandong Foreign Trade Vocational, kilichopo Mkoa wa Shandong, China.

Amesema uhusiano wa nchi hizo ambao uliasisiwa na Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Mwenyekiti Mao Zedong, umeendelea kudumu kutokana na misingi ya kuheshimiana, kutokuingiliana katika mambo ya ndani, na kusaidiana kwa faida ya pande zote.

“Urafiki wetu si wa majira fulani, bali ni wa kudumu. Ushirikiano wa CCM na CPC unapaswa kuwa mfano wa mshikamano wa kweli katika enzi za mabadiliko ya kidunia,”amesema.

Aidha, ameeleza mafanikio ya ushirikiano huo hayawezi kutenganishwa na uongozi imara wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na Rais Xi Jinping wa China.

“Rais Samia amekuwa mfano wa uongozi wa kisasa barani Afrika, anaimarisha mageuzi ya kiuchumi, diplomasia, maendeleo na uwazi wa kimataifa.

“Viongozi wa kimataifa wametambua mchango wake mkubwa katika kuipa Tanzania nafasi ya kimkakati duniani,” amesema Gavu.

Akimzungumzia Rais Xi, ameiongoza China kwa mafanikio makubwa ya kiuchumi na kiteknolojia na kuhimiza ushirikiano wa kweli na mataifa mengine kupitia dira ya ‘Belt and Road Initiative.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here