Home AFYA Moi yaandika historia yawa ya kwanza Afrika kuendesha mafunzo maalum ya upasuaji...

Moi yaandika historia yawa ya kwanza Afrika kuendesha mafunzo maalum ya upasuaji wa mishipa ya damu kwenye ubongo

Dar es Salaam

BAADA ya kuandika historia kwa upasuaji wa kutumia akili unde, sasa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imeandika historia nyingine ya kuwa ya kwanza barani Afrika kuendesha mafunzo maalum ya upasuaji wa mishipa ya damu kwenye ubongo pamoja na magonjwa kwenye sakafu ya ubongo.

Mafunzo hayo yamezinduliwa leo Mei 18, 2025 katika ukumbi wa Ummy Mwalimu na Mkurugenzi wa Tiba Wizara ya Afya, Dk. Hamadi Nyembea ambaye amesema mafunzo hayo ni mara ya kwanza kufanyika Afrika na yatatolewa na wawakilishi wa Shirikisho la Wataalam wa Mifumo ya Fahamu kutoka Nchi za Umoja wa Ulaya(EANS).

“Tumekutana hapa siku ya leo kwaajili ya uzinduzi wa mafunzo maalum ambayo yanahusu upasuaji wa mishipa ya damu kwenye ubongo pamoja na upasuaji wa magonjwa kwenye sakafu ya ubongo na nchi 17 za Afrika zimeshiriki katika mafunzo haya ambayo yanafundishwa na wataalam wa Shirikisho la mifumo ya fahamu kutoka nchi za umoja wa Ulaya( EANS),” amesema Dk. Nyembea.

Dk. Nyambea amesema mafunzo hayo yamekuja kipindi sahihi kwani Serikali tayari imeshawekeza kwa kiasi kikubwa katika huduma za kibingwa na kibobezi zinazopatikana Tanzania.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Balozi Dk. Mpoki Ulisubisya amesema Taasisi ya MOI imekuwa na ushirikiano makubwa na Taasisi na wataalam mbalimbali kutoka nje ya nchi yaliyopelekea MOI kuwa kitovu cha mafunzo ya kibobezi yanayosaidia kutoa huduma bora kwa wangonjwa wanaotibiwa MOI.

Naye, Mwenyekiti wa Shirikisho la Wataalam wa Mifumo ya Fahamu kutoka Nchi za Umoja wa Ulaya, Profesa Magnus Tisell amesema waliichagua MOI kwasababu upasuaji wa mishipa ya damu kwenye ubongo na upasuaji wa magonjwa kwenye sakafu ya ubongo ni aina ya juu zaidi ya upasuaji na MOI imeshawekeza vya kutosha kwenye upasuaji huo.

Mshiriki wa mafunzo hayo kutoka Uganda Dk. Blessing Michael amesema amefurahi kushiriki mafunzo hayo kwani yatamuongezea mbinu mpya za kibingwa na kibobezi za matibabu hayo.

Mafunzo hayo yameratibiwa na Shirikisho hilo kwa kushirikiana na Taasisi ya MOI na yanafanyika kwa siku tano kuanzia leo Mei 18, 2025 na kufikia tamati Mei 22, 2025 katika Taasisi ya MOI, Dar es Salaam.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here