Home KITAIFA Rais Samia awaonya wanaotaka kuvuruga amani

Rais Samia awaonya wanaotaka kuvuruga amani

Na Esther Mnyika, Lajiji

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amezielekeza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Mambo ya Ndani, pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua madhubuti dhidi ya watu wanaotumia vibaya mitandao na teknolojia, huku akitoa onyo kali kwa wanaharakati kutoka nje ya nchi wanaojaribu kuingilia masuala ya ndani ya Tanzania.

Akizungumza leo Mei 19, 2025, wakati wa uzinduzi wa toleo jipya la Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 (toleo la mwaka 2024), Rais Samia amesema sera hiyo imeboreshwa na sasa ina misingi minane badala ya saba, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuiwezesha Tanzania kunufaika zaidi kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni.

Amesisitiza kuwa Tanzania haitakuwa “shamba la bibi” ambapo kila mtu anaweza kuja na kusema au kufanya atakavyo, akionya kuwa kuna baadhi ya wanaharakati kutoka nje ya nchi waliodhibitiwa kwao na sasa wanatafuta pa kupumulia kwa kuvamia nchi nyingine.

“Tumeanza kuona mwenendo wa wanaharakati ndani ya ukanda huu wakianza kuvamia na kuingilia mambo yetu. Kama kwao wameshadhibitiwa, basi wasitafute pa kutuharibia hapa. Nawaomba vyombo vyetu vya ulinzi na usalama wasitoe nafasi kwa watovu wa adabu wa nchi nyingine kuja kutuvuruga,” alisema Rais Samia.

Ameongeza kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakimsema vibaya kupitia mitandao, wakimshutumu kwa ubaguzi na mambo mengine, lakini alisisitiza kuwa analinda maslahi ya nchi na hilo ni jukumu lake kama kiongozi wa taifa.

“Nimeona clip kadhaa za kunisema kuwa nina ubaguzi na mambo mengine. Ninachofanya ni kulinda nchi yangu, na huo ndiyo wajibu wangu. Hatutatoa nafasi kwa kiumbe yeyote, wa ndani ama kutoka nje, kuja kutuvuruga,” alisema kwa msisitizo.

Katika hatua nyingine, Rais Samia ameitaka Wizara ya Mambo ya Nje pamoja na maafisa wake kutoa ufafanuzi wa wazi kwa umma kuhusu tuhuma au hoja mbalimbali zinazotolewa na wanaharakati au watu wengine, hasa kama zina maslahi ya taifa.

Aidha, amezielekeza wizara na wadau wa sera hiyo kuandaa mafunzo ya kina kwa taasisi za umma kuhusu maudhui ya sera hiyo mpya na namna inavyogusa majukumu yao ya kila siku, huku akiwataka mabalozi wa Tanzania walioko nje ya nchi kuisoma, kuielewa na kuitangaza kwa lengo la kuonyesha sura mpya ya diplomasia ya taifa.

Ameeleza kuwa uzinduzi huo ni hatua ya kihistoria inayotokana na maelekezo aliyoyatoa Bungeni Aprili 2021, ambapo maboresho hayo ni matokeo ya mabadiliko makubwa ya kimataifa na kitaifa yaliyotokea katika kipindi cha zaidi ya miaka 20.

Katika hafla hiyo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewataka Watanzania kuitumia sera hiyo kama nyenzo ya kuitetea Tanzania kimataifa na kukuza ushirikiano wa kikanda na kimataifa kwa ajili ya maendeleo ya taifa.

Awali, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabiti, amesema sera hiyo mpya imejikita katika vipaumbele vya kulinda maslahi ya taifa, kuimarisha nafasi ya Tanzania kimataifa kupitia diplomasia ya uchumi, pamoja na kukuza ushirikiano na mataifa mengine na taasisi za kimataifa.

Amesema sera hiyo pia inatambua nguvu ya lugha ya Kiswahili kama bidhaa ya taifa na kwamba Watanzania waishio ughaibuni sasa wanapewa nafasi maalum kwenye ajenda ya kidiplomasia ya taifa.

“Leo tumefanikisha uzinduzi wa sera mpya ya Mambo ya Nje. Sera hii inalenga kuiwezesha Tanzania kuhimili mahitaji mapya ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, huku tukitambua nafasi ya kila Mtanzania, ndani na nje ya nchi, katika kulijenga taifa letu,” alisema Waziri Thabiti.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here