Na Esther Mnyika, Lajiji
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania na Namibia zimekubaliana kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, hususan katika maeneo ya biashara, uwekezaji, nishati, kilimo na sekta ya viwanda, ili kuendeleza maendeleo ya wananchi wa mataifa hayo.

Akizungumza jana Mei 20, 2025 jijini Dar es Salaam mara baada ya mazungumzo yake na Rais wa Jamhuri ya Namibia, Netumbo Nandi-Ndaitwah, Rais Samia alisema licha ya ongezeko la biashara kati ya nchi hizo kutoka Sh bilioni 17 mwaka 2019 hadi Sh bilioni 20 mwaka 2023, kiwango hicho bado ni kidogo na kinahitaji kuongezeka zaidi.
“Tumehimiza mawasiliano ya karibu kati ya sekta binafsi, na tumewaagiza mawaziri wa pande zote mbili kuandaa mikutano ya mara kwa mara ya wafanyabiashara,” amesema Rais Samia.
Aidha, alialika wafanyabiashara wa Namibia kushiriki Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam mwaka huu ili kujifunza na kubadilishana uzoefu.
Kwa upande wake, Rais Nandi-Ndaitwah amesema wamekubaliana kushirikiana katika sekta ya nishati, uchumi wa buluu, na kuongeza thamani ya bidhaa za kilimo, huku akiahidi kutuma mawaziri wake kuja kujifunza Tanzania na kuwahamasisha wafanyabiashara wa Namibia kushiriki maonesho hayo.