Home KITAIFA Wiki ya Azaki kufanyika Juni 2 hadi 6 mwaka huu Arusha

Wiki ya Azaki kufanyika Juni 2 hadi 6 mwaka huu Arusha

Dar es Salaam

MAADHIMISHO ya wiki ya Asasi za Kiraia (Azaki) kwa mwaka 2025 yanatarajiwa kufanyika kuanzia Juni 2 hadi 6 Jijini Arusha yanayolenga kutathimini mafanikio ya Azaki na kupanga mikakati ya kuimarisha maendeleo ya taifa kupitia ushirikiano wa kijamii na kiuchumi.

Akizungumza Mei 22 2025 na waandishi wa habari kuelekea maadhimisho hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, Nesia Mahenge, amesema maadhimisho hayo yatakutanisha wadau mbalimbali kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

kuwa tukio hilo litakuwa jukwaa muhimu kwa wadau kubadilishana uzoefu na kujadiliana kuhusu namna bora ya kushirikiana katika

“Tunashirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo wa serikali, sekta binafsi na washirika wa maendeleo ili kuhakikisha kuwa rasilimali zinazotolewa zinawanufaisha wananchi kwa njia endelevu na shirikishi na kujaduliana kuhusu namna bora ya kushirikiana katika maendeleo endelevu,” amesema Mahenge.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa FCS, Justice Rutenge, amebainisha kuwa hii ni mara ya saba mfululizo kwa Wiki ya Azaki kufanyika, huku mwaka huu ikiambatana na kaulimbiu isemayo: “Njia gani tunaweza kutumia ili kufikia maendeleo.”

Ameeleza kuwa Azaki zimekuwa na mchango mkubwa katika maandalizi ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050 ambayo tayari imekabidhiwa serikalini na inasubiri kuzinduliwa rasmi.

“Azaki zimekuwa mstari wa mbele katika kuchangia mawazo, kushiriki kikamilifu na kuhakikisha kuwa dira hiyo inaakisi matarajio na mahitaji halisi ya Watanzania,” amesema.

Maadhimisho ya mwaka huu pia yataangazia masuala ya utawala bora, uwajibikaji, utoaji wa huduma bora kwa jamii, ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi, pamoja na maendeleo jumuishi.

Pia kutakuwa na mikutano ya kitaalamu, warsha za kujengeana uwezo, kliniki za maarifa na mijadala ya wazi inayowaleta pamoja wadau kutoka nyanja mbalimbali.

Katika hatua nyingine, Benki ya Stanbic Tanzania imetangaza kudhamini maadhimisho hayo kwa kuchangia shilingi milioni 40. SOMA: Watu 500 kushiriki wiki ya Azaki

Akizungumza kwa niaba ya benki hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Taasisi za Umma na Mashirika Binafsi, Doreen Dominic, alisema udhamini huo unaakisi dhamira ya benki hiyo katika kusaidia maendeleo shirikishi.

“Huu ni mwaka wa nne mfululizo tunashirikiana na Azaki, na tunaamini kuwa maendeleo ya kweli yanatokana na mazungumzo ya wazi, ushirikiano na kuaminiana,” amesema Dominic.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tanzania Bora Initiative, Ismail Biro, amesema wiki hiyo itaangazia pia changamoto zinazozikumba Azaki na njia bora za kuzitatua kwa ushirikiano wa wadau mbalimbali, huku makundi maalum kama vijana, wanawake na watu wenye ulemavu yakipewa kipaumbele.

FCS imehimiza washiriki kujisajili mapema ili kuhakikisha wanapata fursa ya kushiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo ambayo yanatarajiwa kuwa jukwaa muhimu kwa wote wenye nia ya dhati ya kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya taifa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here