Home KITAIFA Dk. Samia: CCM itazindua Ilani mpya ya Uchaguzi kesho

Dk. Samia: CCM itazindua Ilani mpya ya Uchaguzi kesho

Na Esther Mnyika, Dodoma

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan amesema chama hicho kipo tayari kuzindua Ilani yake ya Uchaguzi kwa kipindi cha 2025-2030, huku akisisitiza kuwa maandalizi yake yamefanywa kwa umakini mkubwa kwa kuzingatia maoni ya wananchi, asasi na makundi mbalimbali ya kijamii.

Akizungumza leo Alhamisi, Mei 29, 2025 katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu wa CCM, Rais Samia amesema ilani hiyo itazinduliwa rasmi kesho Mei 30, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.

“Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa 2025 inaakisi kipindi cha pili na cha mwisho cha utekelezaji wa sera za CCM kwa miaka 2025 hadi 2030. Tumeona ni muhimu kabla hatujaifikisha kwa wananchi tufanye mapitio ya ilani iliyopita ya mwaka 2020-2025 na hiyo ndiyo kazi tuliyoifanya leo,” amesema.

Ameeleza kuwa matarajio yake ni kuona wajumbe wa mkutano huo wanakuwa mabalozi wa kuipeleka ilani hiyo kwa wananchi na kuisimamia katika utekelezaji wake pindi CCM itakapopewa ridhaa ya kuongoza tena.

“Ilani hii imeandaliwa kwa weledi mkubwa na kuhusisha wananchi wenyewe, asasi za kiraia, makundi ya kijamii na vipaumbele vya chama. Inalenga kuhakikisha maendeleo yanamfikia kila Mtanzania,” amesema Samia.

Aidha, Samia amesema jana aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa Makao Makuu ya CCM mkoani Dodoma, jengo litakalogharimu Shilingi bilioni 34 na linatarajiwa kukamilika Mei 20, 2027, sambamba na maadhimisho ya miaka 50 ya CCM.

Kuhusu vikao vya chama, Rais Samia amesema Mkutano Mkuu Maalumu uliofanyika Januari 18 na 19, 2025, ulishughulikia taarifa ya utekelezaji wa shughuli za chama kwa miaka miwili (2022-2024), utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya 2020-2025, pamoja na kufanya marekebisho madogo ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977.

Vilevile, mkutano huo ulimaliza kazi ya kumteua mgombea urais wa Tanzania, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi pamoja na mgombea mwenza wake, na kumthibitisha Dk. Hussein Mwinyi kuwa mgombea wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM kuelekea Uchaguzi Mkuu.

Amesema Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM katika kikao chake cha Machi 2025 ilipokea na kuridhia Ilani ya Uchaguzi ambayo itazinduliwa rasmi kesho, tayari kwa kuwasilishwa kwa wananchi.

“Mkutano huu ni sehemu muhimu ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2025. Ni fursa ya kutathmini yaliyofanyika na kujiandaa kwa hatua zinazofuata,” amesema.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi amesema mkutano huo ulikuwa na agenda tatu kuu: kupokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya 2020-2025, kuzindua Ilani ya 2025-2030 na kufanya marekebisho madogo ya Katiba ya chama.

Katika mkutano huo, wajumbe 1,907 walihudhuria, sawa na asilimia 98.6 ya waliotarajiwa, huku wajumbe 27 wakitoa udhuru. Rais Samia pia alitangaza kuwa idadi ya wanachama wa CCM imeongezeka kutoka milioni 12 katika mkutano mkuu uliopita hadi kufikia milioni 13 hivi sasa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here