*Dk Mwinyi ameweka alama ya kipekee Zanzibar
Na Esther Mnyika, Lajiji-Dodoma
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imetekeleza kwa mafanikio makubwa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020/2025, huku akisisitiza kuwa maendeleo yaliyopatikana yamewagusa wananchi katika kila kona ya visiwa hivyo.
Akizungumza Mei 29, 2025, katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma, Hemed akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani hiyo kwa upande wa Zanzibar, alisema miradi ya maendeleo iliyotekelezwa imevuka malengo katika nyanja za kijamii, kiuchumi na kisiasa.

“Ilani haikutekelezwa tu kama ilivyoelekezwa, bali mengine yamefanyika zaidi ya ilivyopangwa. Hili si tu linashuhudiwa na wanachama wa CCM, bali na wananchi wote wa Zanzibar,” alisema Hemed.
Akimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, Hemed alisema Serikali ya Awamu ya Nne ya Zanzibar imeweka alama ya kipekee katika historia ya utekelezaji wa Ilani, kiasi kwamba Oktoba 2025, Wazanzibari watatoa kura za kishindo kuthibitisha imani yao kwake.
“Shehia zote za Zanzibar zimeguswa. Hakuna aliyebaki nyuma. Miradi ya elimu, afya, maji, barabara, michezo na hata uanzishaji wa viwanda imefika kila pembe ya Visiwa vya Unguja na Pemba,” alisema.
Amesema kuwa kupitia miradi ya kimkakati ya kilimo na viwanda, SMZ imefanikiwa kuunganisha wananchi wa Zanzibar katika wilaya zote 11 za Serikali na wilaya 12 za kichama, huku akisisitiza kuwa mafanikio hayo ni ushahidi wa dhamira ya dhati ya CCM katika kuinua maisha ya wananchi.
Katika sekta ya michezo, Hemed alitaja maendeleo ya viwanja vya kisasa kama Uwanja wa Amani, akitoa mfano wa namna uwanja huo ulivyokuwa kitovu cha fursa za kiuchumi wakati wa mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika kati ya Simba na Berkane ya Morocco.
“Wakati ule hoteli zote zilijaa, mji ulikuwa hauna nafasi. Baadhi ya watu walihama nyumba zao kuzipangisha na kwenda kwa ndugu zao vijijini – hiyo ndiyo fursa ya kiuchumi tuliyoipata kupitia uboreshaji wa miundombinu,” alieleza.
Kwa upande wa elimu, alibainisha kuwa shule za ghorofa zimejengwa kwa mara ya kwanza visiwani humo, hatua inayolenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuongeza udahili wa wanafunzi.
Akimalizia hotuba yake, Hemed aligusia pia taswira ya Zanzibar kimataifa, akisema kuwa mageuzi ya kiuchumi na kijamii yanayoendelea yanaifanya Zanzibar kuwa kivutio si tu kwa wawekezaji bali pia kwa mashindano makubwa ya michezo na sekta ya utalii.

Katika mkutano huo, Hemed pia alitania hali ya ushindani kati ya timu za Simba na Yanga katika michuano ya Afrika, akisema kuwa licha ya Simba kushindwa kuacha kombe nyumbani, ipo siku Yanga italibakisha nchini.
Mkutano huo wa CCM Taifa ni sehemu ya maandalizi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025, ambapo Ilani mpya ya mwaka 2025/2030 inatarajiwa kuzinduliwa rasmi.