Na Esther Mnyika, Dodoma
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, ametoa wito mzito kwa vikao vya chama hicho vinavyosimamia mchakato wa kuwachuja wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi kuhakikisha vinafanya kazi hiyo kwa haki, umakini na uadilifu mkubwa, bila upendeleo wala kuoneana haya.
Akihitimisha Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM Taifa uliofanyika kwa siku mbili jijini Dodoma leo Ijumaa, Mei 30, 2025, Rais Samia amesema ni muhimu kwa vikao hivyo kutenda haki kwa kila mwanachama, kwa kuzingatia sifa, uwezo na maadili ya wagombea badala ya misukumo ya kisiasa au makundi.
“Vikao vinavyokwenda kuchuja wagombea vitende haki. Anayefaa aambiwe anafaa, asiyefaa aambiwe huyu anakasoro mbili, tatu, hatufai huko tunakokwenda. Tukitoa mwanya, tukapitisha wanaotutafuta tu — nami niwemo — ndiyo tunapata wale wanaokwenda huko, chama kinakuwa Gwajimanized,” alisema Rais Samia huku akishangiliwa na wajumbe wa mkutano huo.

Alifafanua kuwa iwapo chama kitashindwa kuwa makini katika hatua hii ya awali ya mchakato wa uchaguzi, kuna uwezekano mkubwa wa kupenyezwa kwa watu wasiofaa, ambao baadaye wanaweza kuwa chanzo cha migogoro, migawanyiko na kushuka kwa hadhi ya chama hicho kikongwe barani Afrika.
“Kwa vyovyote vile, tusikubali chama chetu kigwajimanizwe. Magwajima tuyatupe nje, hatuna muda wa mzaha. Hii ni kazi ya kitaasisi, siyo ya mihemko wala ushabiki wa kisiasa,” aliongeza kwa msisitizo.
Katika hatua nyingine, Rais Samia alieleza bayana kuwa yeye pamoja na mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dk. Hussein Ali Mwinyi, hawajamtuma mtu yeyote kugombea jimbo lolote nchini, na kwamba mtu yeyote anayejinadi kuwa ametumwa na viongozi hao, jina lake liondolewe mapema kutoka kwenye orodha ya wagombea.
“Sisi tunazo nafasi zetu kumi kumi. Baada ya uchaguzi, wale tunaowataka ndiyo tutakaowapa hizo nafasi. Kwa hiyo, mlio kwenye majimbo mjizatiti huko huko, msifanye kwa uwoga. Huu ni uwanja wazi — kila mtu ajipime uwezo wake, aingie kwenye mchezo. Hakuna anayezuiwa. Wananchi wataamua nani wanamtaka,” alisema.

Rais Samia pia alielekeza kuwa ifikapo Juni 1, 2025, CCM iwe imeshapokea majina ya watu wote wanaotaka kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, hatua ambayo inalenga kutoa muda wa kutosha kwa Kamati za Siasa na vikao husika kufanya kazi yao kwa weledi, umakini na bila presha ya muda.
“Wale walioko kwenye vikao vya uchujaji lakini pia wana nia ya kugombea, tunaomba watoe taarifa mapema. Ukichelewa hadi uchukue fomu tayari, utakuwa umesababisha usumbufu kwa wengine na kuathiri mchakato mzima,” alieleza.
Aidha, Rais Samia aliwasihi wajumbe wa CCM kuendeleza mshikamano, maelewano, upendo na uzalendo ndani ya chama, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, ili chama kiendelee kuwa imara na cha kuaminika kwa wananchi.
“Chama hiki ni taasisi kubwa. Tusiingize makundi, fitna wala mizengwe. Huu ni wakati wa kukijenga chama, si kukibomoa. Tushirikiane, tukosoane kwa heshima, lakini tusibomoe msingi uliotupeleka hapa tulipo,” alisisitiza.
Mkutano huo wa CCM Taifa umehudhuriwa na viongozi wakuu wa chama hicho kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar, wakiwemo wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), wakuu wa mikoa, makatibu wa chama, wabunge, wawakilishi na viongozi waandamizi wa serikali.
Mkutano huo pia umetumika kuzindua rasmi Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025–2030, iliyoeleza vipaumbele vyake katika kukuza uchumi, ajira, ustawi wa jamii, miundombinu, demokrasia na utawala bora.