Dodoma
WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso amewataka Watanzania kuendelea kutunza mazingira pamoja na kuendeleza vyanzo vya maji ili kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji na uzalishaji wa nishati ya nguvu ya umeme, ambayo ni mihimili muhimu katika kukuza uchumi wa nchi na wananchi kwa ujumla.

Amesema hayo Juni, 2 2025 jijini Dodoma Aweso alipotembelea mabanda ya maonesho kuelekea maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani Juni 5.
Amesema mabadiliko ya sera ya mazingira yaliyofanywa na serikali yanalenga kuendana na matakwa ya kimataifa.
“Mabadiliko haya yamefungua fursa kwa serikali kushirikiana na wadau mbalimbali katika kulinda mazingira, ili kuhakikisha Tanzania inakuwa salama na yenye ustawi wa kijamii na kiuchumi,”amesema.

Aweso amewahimiza wananchi kuendelea kutunza na kuendeleza vyanzo vya maji, akisisitiza kuwa ni msingi wa upatikanaji wa chakula na utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya taifa.
Amesema kuwa wananchi wanapaswa kubadilika na kuachana na tabia zinazoharibu mazingira, ikiwa ni pamoja na matumizi holela ya plastiki ambayo yamekuwa chanzo kikuu cha uharibifu wa mazingira.

Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka ni: “Tanzania Ijayo, Tuwajibike Sasa Dhibiti Matumizi ya Plastiki.”