▪️Ataka jamii na vijana washirikishwe kwenye biashara ya kaboni
Dar es Salaam
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amezitaka halmashauri zote nchini zihakikishe kuwa zinaweka vituo vya kuchakata na kutenganisha taka ili zinapozalishwa ziweze kushughulikiwa kwa njia salama na endelevu, kwa lengo la kupunguza mzigo wa taka unaokwenda majalalani au kusambaa ovyo katika makazi ya watu.

Pia amezitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa zishirikiane na Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira kuandaa mipango ya kuwezesha jamii na vijana kushiriki biashara ya kaboni, kutumia na kuendeleza teknolojia za nishati safi na miradi ya urejelezaji wa taka (recycling).
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo Juni 3, 2025alipozungumza na vijana katika Jukwaa la Vijana na Mazingira lililofanyika katika Ukumbi wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo hufanyika Juni 5 kila mwaka ambapo kitaifa yatafanyika Jijini Dodoma.
Waziri Mkuu amesema jukwaa hilo la vijana na mazingira linalenga kuwaunganisha vijana kutoka sehemu mbalimbali nchini na kuwajengea uelewa kuhusu masuala ya utunzaji wa mazingira pamoja na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika kubuni na kutekeleza mikakati ya kutatua changamoto za mazingira nchini.

Amesema ni vizuri uhamasishaji wa kuendeleza Kampeni ya Usafi wa Mazingira inayofanyika kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi uimarishwe kwa wananchi na jamii na sekta binafsi nayo iweke mifumo ya urejelezaji wa taka zinazotokana na shughuli za viwanda Ili kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa haziishii kuharibu mazingira.
“Tunavyoelekea kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani tarehe 5 Juni, 2025, ni muhimu kwa vijana kutambua nafasi yenu kwenye agenda ya mazingira kupitia jukwaa hili. Jukwaa hili la vijana na mazingira linapaswa kuwa chachu ya kuibua ubunifu, kuongeza uelewa na kushirikisha nguvu kazi ya Taifa katika kulinda na kuhifadhi mazingira yetu,”amesema.
Akizungumzia kuhusu mikakati ya Serikali ya kulinda mazingira, Waziri Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ambapo zaidi ya taasisi 762 zimekwisha anza kutumia nishati mbadala. Malengo ni kufikia asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi kufikia mwaka 2034.
Amesema katika upandaji miti, mwaka 2023/2024, zaidi ya miti milioni 266 ilipandwa, pamoja na juhudi za kupanda miti bado Taifa linakabiliwa na changamoto ya upotevu wa misitu inayokadiriwa kufikia hekta 469,420 kwa mwaka, ambapo Serikali imefanikiwa kuweka msukumo katika ushiriki wa vijana katika shughuli za mazingira.

“Usafi wa mazingira na udhibiti wa taka ni moja ya changamoto za kimazingira zinazohitaji hatua za makusudi na za haraka. Takwimu zinaonesha kuwa, takribani kiasi cha tani millioni 14.4 hadi 20.4 za taka ngumu huzalishwa nchini hususani katika miji mikuu na majiji. Aidha, ni wastani wa asilimia 50 tu ya taka zinazozalishwa hukusanywa na kutupwa ipasavyo,”amesema.
Amesema kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, changamoto hizo ni fursa zinazoweza kutoa ajira kwa vijana, kukuza uchumi na kuongeza kipato kwa kijana mmoja mmoja.
“Hivyo, nitumie fursa hii kuwasihi vijana wote mliopo hapa, kushiriki kikamilifu katika shughuli za uhifadhi na usimamizi wa mazingira kwa kuzingatia kuwa ni fursa ya kuongeza kipato na ajira kwa ujumla,”amesema.

Amesema Mei, 28 2025, Serikali ya Tanzania na Japan ziliingia makubaliano ya ushirikiano katika mpango wa pamoja wa uwekezaji katika biashara ya hewa ya ukaa (kaboni) utakaoongeza fursa ya kupanua soko la biashara hiyo nchini. Aidha, Serikali imenzisha kituo cha Kitaifa cha Ufuatiliaji wa kaboni kupitia sheria ya Usimamizi wa Mazingira iliyofanyiwa marekebisho ya Mwaka 2025. “Hii ni hatua nyingine ya Serikali ya kusahirikiana na wadau wa mazingira.”
Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Hamza Khamis amesema Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira imeweka jitihada kubwa za utunzaji wa mazingira ambapo imeelekeza kila halmashauri kupanda miti isiyopungua milioni 1.5 kila mwaka.
Pia, Naibu Waziri huyo amesema Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kuibua fursa zitokanazo na masuala ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira kama biashara ya kaboni, urejeshaji wa taka pamoja na kuandaa kanuni, mikakati na miongozo mbalimbali ya usimamizi wa mazingira ukiwemo muongozo wa 3R yaani punguza, tumia tena na rejeleza wenye lengo la kuimarisha na kusimamia taka nchini.
“Tulikuwa tunasema taka ni uchafu ila sasa taka ni utajiri na taka ni suluhisho la vijana kwenye mazingira.”