📌 Tanga kuwa Kitovu cha Nishati nchini
📌 Dkt. Biteko Asisitiza Ajira Kwa Wazawa
📌Kampeni ya Rais Samia ya Nishati Safi ya Kupikia Yavutia Wawekezaji
📌Matumizi ya Gesi ya Kupikia Yaongezeka Kila Mwaka
Tanga
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko ametoa wito kwa wawekezaji nchini kutoa kipaumbele cha ajira kwa Watanzania ili kukuza kipato cha mtu mmoja mmoja na uchumi wa Taifa kwa ujumla.

Amewaomba wawekezaji wa mradi wa Kituo cha Gesi cha Tanga International Energy licha ya kuwa zitazalishwa ajira zaidi ya 300 na baadae zaidi ya 2,000, waangalie utaratibu katika ujenzi wa mradi huo ambao utawezesha wazawa kupata kazi na hakuna sababu ya kutafuta watu kutoka mbali.
Dk. Biteko ametoa wito huo leo Juni 5, 2025 jijini Tanga wakati akimwakilisha Rais wa Dk. Samia Suluhu Hassan katika ujenzi wa Kituo cha Gesi cha Tanga International Energy mkoani humo.
“Mradi huu uwe mfano wa kielelezo kila kazi anayoweza kufanya Mtanzania apewe, ili asilimia 40 ya fedha za ujenzi wa mradi zizunguke nchini. Nitasikitika nikiona kila aina ya kazi analetwa mtu kutoka nje kuja kufanya,” amesema Dk. Biteko.
Ameendelea kutoa wito kwa wawekezaji kufikiria namna ya kupeleka huduma ya ujazaji mitungi ya gesi katika maeneo ya vijijini ikiwa ni pamoja na kuanzisha teknolojia ya kusaidia mtu aweze kulipia gesi kulingana na mahitaji yake badala ya kujaza mtungi mzima.

Dk. Biteko amesema kwa mujibu wa taarifa ya utendaji sekta ndogo ya mafuta ya EWURA ya mwaka 2024, matumizi ya gesi ya kupikia yaani (LPG) huongezeka kwa kasi kila mwaka. Ambapo kwa mwaka 2023/24 matumizi yalifikia zaidi ya tani 403,000 ikilinganishwa na tani 293,000 mwaka wa fedha 2022/23 sawa na ongezeko la asilimia 38.
Amewahakikishia Kampuni ya Tanga Energy International Ltd kuwa mradi wao utakuwa na uhakika wa soko ndani na nje ya nchi na kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao ili kufikia malengo yao ya kuleta huduma bora na nafuu kwa Watanzania.
Katika kuthibitisha hilo, Dk. Biteko amesema kupitia Wakala wa Nishati Vijijini, Serikali inaendelea na programu ya kutoa ruzuku ili wananchi wapate mitungi ya gesi ya kupikia kwa punguzo la bei hadi kufikia asilimia 50 na kusambaza mitungi 452,445 ambapo hadi kufikia Aprili, 2025 jumla ya mitungi 154,225 imeshasambazwa.
“ Tarehe 2 Juni, 2025 pale jijini Dodoma tumezindua Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano wa Nishati Safi ya Kupikia. Hivyo, kupitia Mkakati huu, Serikali itaendelea kutoa elimu nchi nzima na hivyo kuinua uelewa wa wananchi na hatimaye kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia ambapo LPG ni chanzo kikuu,” amesisitiza Dk. Biteko.
Katika hatua nyingine, Dk. Biteko amesema Rais Samia anataka Mkoa wa Tanga uwe kitovu cha biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki, na hivyo ameendelea kufanya jitihada mbalimbali ili kutimiza lengo hilo ikiwemo kupanua mfumo wa kusafirisha umeme kutoka Majani mapana hadi Pemba kutoka kilovoti 33 hadi 132.

Pamoja na hayo ametoa wito kwa Watanzania kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu kwa kuchagua viongozi wanaofaa “ Tumuunge mkono Rais Samia kwa kuwa kinara wa Kampeni ya Nishati Safi kimataifa ili Watanzania wengi watumie nishati safi ya kupikia,” amemaliza Dk. Biteko.
Naye, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Suleiman Jafo amesema kuwa utendaji kazi wa Dk. Biteko umesaidia kuimarika kwa sekta ya nishati huku akisisitiza kuwa kukamilika kwa mradi huo mkubwa wa Kituo cha Gesi kutaifanya Tanzania kuwa msafirishaji mkubwa wa gesi na kuchochea ukuaji wa viwanda nchini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Burian amesema mradi huo utasaidia kuitangaza Tanga kimataifa, kuongeza ajira na pato la mkoa na Taifa kwa ujumla.
Akitoa salamu za Chama cha Gesi na Mafuta, Mkurugenzi Mtendaji wa TOAG, Abdulsamad Abdulrahim amesema mradi huo utaisaidia Tanzania kuleta mapinduzi ya nishati katika ukanda wa Afrika Mashariki, kupunguza athari zinazotokana na matumizi ya nishati isiyo safi.

Abdulrahim amebainisha kuwa Watanzania wako tayari na hiyo ni fursa kwa wawekezaji wazawa kuonesha uwezo wao na wako tayari kufanya kazi.
“Tunaishukuru Serikali kwa kuweka mazingira wezeshi ya kusaidia utekelezaji wa miradi kama hii ambayo ni zao la ushirikiano wa wageni na wazawa wenye kufanya mawazo kuwa uhalisia,” amesema Abdulrahim.
Awali akitoa maelezo ya mradi, Michael Dimond amesema LPG ni suluhu ya nishati safi ya kupikia na kuwa Kampuni ya Pretedec imefurahishwa jitihada za Rais Samia katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia na lengo la Serikali la kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
“Leo tunajivunia kuwekwa kwa jiwe la msingi katika mradi huu wa kipekee Tanzania ambao umezingatia usalama wa usambazaji wa LPG katika ukanda wa Afrika Mashariki,” amesema Dimond.
Mwakilishi wa Kampuni ya Asas, Ahmed Asas amesema mbali na manufaa ya kiafya na mazingira mradi huo utachochea uchumi jumuishi na kuchangia katika ukuaji wa viwanda vya ndani.
Mradi wa Kituo cha Gesi cha Tanga International Energy unatekelezwa kwa ushirikiano wa Kampuni ya Pretedec na Asas ambao unatagharimu dola za marekani milioni 100 utakuwa mradi mkubwa wa LPG nchini. Aidha, kupitia mradi huo unaotarajiwa kukamilika 2027 utanufaisha pia nchi za Burundi, Kenya, Uganda, Burundi na Zambia kwa kuagiza gesi kutoka nchini Tanzania.