Home AFYA Mhagama: azindua Bodi ya Wadhamini ya MOI

Mhagama: azindua Bodi ya Wadhamini ya MOI

Dodoma

WAZIRI wa Afya, Jenista Mhagama amezindua Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) na kuitaka bodi hiyo kuimarisha huduma za kibingwa na kibobezi za Taasisi hiyo na kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi wengi zaidi.

Mhagama ameyasema hayo leo Juni 9, 2025 katika ukumbi wa Wizara ya Afya, Dodoma katika tukio la uzinduzi wa bodi hiyo ambapo ameitaka bodi hiyo iende kuimarisha misingi walioyoikuta MOI na kuongeza ubunifu katika kuboresha utoaji wa huduma hizo kwa wananchi.

“Leo ni siku nyingine ya kihistoria tunazindua Bodi mpya ya wadhamini na tunaamini inakwenda kuimarisha huduma ambazo zimeshawekwa, na hatutarajii kuona bodi hii ikaenda kubomoa misingi hiyo na tunachokitazamia kutoka kwenu ni ubunifu zaidi ya hapa tulipofika kwenda mbele,”amesema Mhagama.

Mhagama ameitaka bodi hiyo kuhakikisha huduma za MOI zinawafikia wananchi wenye uhitaji kwani hakutakuwa na faida ya uwekezaji kwenye ubingwa na ubobezi katika sekta hii muhimu kama wananchi wenye uhitaji wa huduma hizo watashindwa kuzipata.

Pia, ameipongeza Taasisi ya MOI jinsi inayoendelea kujipanga katika kuhakisha inaondoa utegemezi katika huduma za kibingwa na kibobezi za matibabu ya mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu kuwapeleka watanzania wengi nje ya nchi na kufanya matibabu hayo yapatikane hapa Tanzania.

Aidha, amemshukuru na kumpongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa ajenda yake ya kitaifa ya kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya afya.

Kwa upande wake Mwenyekiti mpya wa bodi hiyo Dk. Marina Njelekela amesema watahakikisha wanafanya kazi kwa pamoja na kwa ukaribu na Menejimenti ya MOI ili waipeleke MOI mbele zaidi ya hapa walipoikuta.

Pia, Dk. Njelekela ameahidi kutekeleza maagizo yote waliyopatiwa na Mhe Waziri wa Afya ya kuhakikisha huduma za kibingwa na kibobezi MOI zinaendelea kuwa bora na kunufaisha Watanzania na raia wa mataifa jirani.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Balozi Dk. Mpoki Ulisubisya amemshukuru Mhagama kwa kutenga muda wake na kumhakikishia kwamba Management ya MOI itaendelea kuchapa kazi kwa bidii kadri alivyowaelekeza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here