Home MICHEZO Waziri Mkuu: Serikali yatenga shilingi bilioni 43 kuimarisha michezo shuleni

Waziri Mkuu: Serikali yatenga shilingi bilioni 43 kuimarisha michezo shuleni

▪️Azindua mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA Iringa

Iringa

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali imetenga shilingi bilioni 43 ili kuimarisha michezo katika shule mbalimbali nchini na kati ya hizo, shilingi bilioni 32 ni kwa ajili ya kuimarisha Chuo cha Michezo Malya.

Amesema shilingi bilioni 11 zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza mpango wa kuboresha miundombinu ya michezo katika shule za sekondari 10 ambazo ni miongoni mwa shule teule 56 za michezo nchini.

Ametoa kauli hiyo leo Juni 9, 2025 wakati akifungua mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi na Sekondari Tanzania (UMITASHUMTA na UMISSETA) kwenye viwanja vya Kichangani vilivyoko Kihesa, mkoani Iringa.

Akielezea mikakati ya Serikali ya kuendeleza michezo na sanaa nchini, Waziri Mkuu amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imejipanga kuimarisha Chuo cha Michezo Malya ili kiendelee kutoa mafunzo kwa kuzingatia utaalam na kuimarisha ufundishaji wa masomo ya michezo shuleni.

“Chuo hiki kikikamilika kitawanufaisha wanafunzi wanamichezo wanaoonesha vipaji katika mashindano haya,” amesema na kuongeza kuwa mpango huo unatekelezwa kwa lengo la kuweka mazingira mazuri ya michezo na sanaa nchini kwa ajili ya kuandaa wataalam na wanamichezo mahiri.

Amesema Serikali imeendelea kuimarisha michezo katika ngazi zote za elimu ikiwemo kuratibu mashindano ya michezo ya Umoja wa Michezo na Taaluma katika shule za msingi, sekondari na vyuo ili kuibua vipaji vya michezo kuanzia ngazi za chini sambamba na kuanzisha shule za akademia za michezo.

Kuhusu mafunzo kwa walimu wa michezo, Waziri Mkuu amezitaka Halmashauri zote nchini zihakikishe walimu mbalimbali wanahudhuria mafunzo ya michezo katika vyuo mbalimbali ikiwemo Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya ili kupunguza uhaba wa watalaamu wa michezo katika shule mbalimbali na nchini kwa ujumla.

“Wapelekeni walimu katika vyuo vya taaluma kama Malya, Butimba na wale wanaopata sifa za kwenda vyuo vikuu waende wakaimarishe utaalamu wao, ili waalimu hawa wanapopewa timu basi tunakuwa na timu zenye uhakika kwamba zimefundishwa na walimu wenye uwezo ulioimarika,”amesema.

Aidha ameitaka Wizara ya Elimu na Ofisi ya Rais TAMISEMI waimarishe usimamizi ili ratiba za shule zote ziwe na vipindi vya michezo na wahakikishe vipindi hivyo vinatumika kikamilifu.

Akielezea manufaa ya mashindano hayo ambayo yameiwezesha nchi kupata wachezaji wanaofuzu kucheza soka la kulipwa kwenye viwango vya kimataifa, Waziri Mkuu amewataka wanafunzi wanaoshiriki mashindano hayo waongezee bidii ili waweze kuibuka kidedea. Amewataja baadhi wa wanamichezo waliofuzu kuwa ni Mbwana Samatta (Ugiriki), Simon Msuva (Iraq), Novatus Miroshi (Uturuki), Kelvin John (Denmark), Abdi Banda (Afrika Kusini), Adi Yusufu (Uingereza) na Himid Mao (Misri).

Naye Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi amesema mafanikio yanayoendelea kuonekana kwenye sekta ya michezo nchini, ni ushahidi tosha jinsi Serikali ya awamu ya sita ilivyodhamiria kukuza sekta hiyo.

Amesema Serikali imeendelea na ujenzi na ukarabati wa viwanja mbalimbali ikiwa ni maandalizi ya michuano ya CHAN 2025 inayotarajiwa kuanza Agosti 2, mwaka huu. “Serikali inaendelea na ujenzi wa viwanja vya kisasa katika Jiji la Arusha na Jiji la Dodoma. Pia inafanya ukarabati wa viwanja vya mazoezi katika Jiji la Dar es Salaam na Jiji la Arusha na inaendelea pia na ukarabati wa viwanja vya Benjamin na Uhuru jijini Dar es Salaam.”

Naye, Naibu Waziri wa TAMISEMI (Elimu), Zainab Katimba amesema mwaka huu Serikali imetoa shilingi bilioni 2.4 ili kufanikisha mashindano hayo ya UMISSETA NA UMITASHUMTA.

Amesema katika kuboresha shule 26 za amali nchi nzima, Serikali imeanza na mikoa 10 na kwa mkoa wa Iringa, shule za sekondari za Iringa Girls’ na Lugalo zimepatiwa sh. milioni 450 ili kukamilisha ukarabati wa viwanja vya michezo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here