Home AFYA Evelin: Mama anayepambana na mwanaye asiye na jinsia katikati ya umasikini

Evelin: Mama anayepambana na mwanaye asiye na jinsia katikati ya umasikini

Na Esther Mnyika, Lajiji-Dar es Salaam

Katika pembezoni mwa jiji la Dar es Salaam, ndani ya nyumba ya bati iliyochakaa kwenye mtaa wa Mkamba, kata ya Kisarawe II, kuna maisha yanayosimulia hadithi ya uchungu, imani na matumaini ya mama mmoja kwa mtoto wake wa kipekee. Evelin John (35), mama wa watoto sita, anapambana kila siku kuhakikisha mtoto wake wa tano, Imani John(7) siyo jina lake halisi, ambaye alizaliwa bila jinsia ya kike wala ya kiume, anaendelea kuishi licha ya changamoto zinazomzingira.

Imani alizaliwa mwaka 2018 akiwa tofauti. Hakuwa na viungo vya uzazi vinavyotambulika kwa jinsia ya kiume au ya kike. Kwa mujibu wa vipimo vya madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Imani ana homoni za kiume, lakini kimwili hakuendelezwa kama mvulana wala msichana. Ndiyo maana aliitwa jina la kiume, ingawa mwonekano wake hauna mwelekeo wa moja kwa moja wa kijinsia.

Maisha yasiyo ya kawaida

Katika mazungumzo maalum na Lajiji Digital, iliyofunga safari hadi nyumbani kwa mama huyu, anasimulia kwa uchungu jinsi mtoto wake anavyopitia mateso yasiyoelezeka kila siku. “Mtoto wangu hana sehemu rasmi ya kutoa haja ndogo au kubwa. Anatoa haja ndogo upande wa kushoto wa mwili, na haja kubwa anatobolewa upande wa kulia chini ya mbavu. Katika msimu wa baridi, hulia sana, anasema ‘mama naumia, nasikia uchungu,’” anasema Evelin huku sauti yake ikikata kwa huzuni.

Kila baada ya dakika chache, Imani huhitaji kubadilishwa nguo kutokana na hali hiyo. Kwa familia isiyo na uwezo hata wa kupata pakiti ya pempasi, hili limekuwa jambo gumu.

“Hali ya maisha ni ngumu sana. Sina uwezo wa kumpeleka hospitali wala kumudu bima ya afya. Kwa zaidi ya miaka miwili sasa hajafanyiwa kliniki yoyote, na vifurushi vya bima vimepanda bei kiasi kwamba hatuwezi kumudu.”

Kutengwa na kupambana peke yake

Mbali na changamoto za kiafya na kiuchumi, Evelin anakumbana pia na changamoto ya kijamii. Wakati baadhi ya ndugu wakiwa wamemgeuka, akihusishwa na “laana” au mkosi, jamii inayomzunguka imempa faraja kiasi.

“Wapo ndugu walionitenga kwa sababu ya hali ya mwanangu. Wananiona kama nilifanya dhambi au kosa. Lakini majirani wangu wamekuwa msaada mkubwa, walau wananitia moyo,” anasema Evelin.

Imani anapenda shule, lakini…

Ingawa Imani ni mtoto mwenye akili nzuri na anayependa shule kwa dhati, bado hajaanza masomo rasmi. Walimu katika shule ya karibu walishauri mzazi awepo muda wote kumsaidia wakati wa kubadilishwa nguo, jambo ambalo familia hiyo haiwezi kutekeleza kutokana na hali ya kiuchumi.

“Kuna wakati ananiuliza: ‘Mama, mbona siendi shule wakati mimi ni mkubwa? Watoto wanaenda shule na mimi nabaki nyumbani.’ Moyo wangu huuma sana,” anasema Evelin kwa uchungu mkubwa.

Wito kwa Rais na Watanzania wote

Evelin anaelekeza wito wake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, pamoja na watanzania wenye moyo wa huruma na wadau wa afya, kusaidia kupata matibabu na bima ya afya kwa mtoto wake.

“Namwomba Mama Samia anisadie, mwanangu apate matibabu. Aishi maisha ya kawaida kama watoto wengine. Pia natamani awe na bima ya afya, kwani hata huduma ndogo hatuwezi kuipata,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mkamba, Mussa Mohamed, amethibitisha kuwapo kwa mtoto huyo na juhudi za kutafuta msaada.

“Ni kweli Imani ana changamoto hiyo. Tumeanza jitihada za kumsaidia lakini tunahitaji msaada zaidi. Tunawaomba watu wenye moyo wa huruma wajitokeze,” amesema mwenyekiti huyo.

Tuungane kumsaidia Imani

Watanzania wote wenye moyo wa huruma na taasisi zinazojali haki za watoto wanahimizwa kujitokeza kumsaidia mtoto huyu apate matibabu na elimu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here