Dar es Salaam
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali itaendelea kuiimarisha Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) ili ifikie maono ya kuwa kitovu maridhawa cha ubora katika uandaaji, ukuzaji na ubunifu wa mitaala.

Amesema kuwa TET ni moyo wa ukuaji wa elimu nchini na hasa kwa kuwa ndiyo inayojenga msingi wa elimu kuanzia Darasa la Awali mpaka Kidato cha Sita.
Amesema hayo leo Jumanne Juni 17, 2025 alipomwakilisha Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika kilele cha Maadhimisho ya Miaka 50 ya Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) yanayofanyika katika viwanja vya Taasisi hiyo, Bamaga Jijini Dar es Salaam.
“Serikali inatambua wakuza mitaala wanafanya kazi kwa bidii, weledi, maarifa na moyo wa kizalendo sana. Hivyo, niwahakikishia Watanzania wote kuwa, wakati wote Serikali, itaendelea kuimarisha utendaji wa TET ili kwenda sambamba na kazi ya ukuaji wa sayansi na teknolojia,”amesema.

Katika hatua nyingine, Majaliwa ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iimarishe ushirikiano na taasisi nyingine za ndani na nje ya nchi ili TET ipate uzoefu zaidi katika kuandaa mitaala, kuandaa vifaa vya mtaala na kutoa mafunzo endelevu ya walimu kazini.
“Hii inamaana ya kuwepo kwa ziara za ndani na nje ya nchi kwenda kupata uzoefu, msijifungie hapa tu, nendeni mkaone wenzenu wanafanya nini, ili muendelee kufanya maboresho zaidi kwenye taasisi yenu,”amesema.
Ameeleza mafanikio kadhaa yaliyopatikana katika masuala ya uandaaji wa mitaala, vitabu vya kiada na vifaa vingine vya utekelezaji wa mitaala, matumizi ya TEHAMA na teknolojia nyingine katika utoaji wa huduma zenu pamoja na utoaji wa mafunzo kwa walimu na wasimamizi wa utekelezaji wa mitaala.

Aidha, Majaliwa ameipongeza taasisi hiyo kwa mapinduzi makubwa ya matumizi ya TEHAMA na mifumo wa kidijitali. Katika hili nimejionea mwenyewe katika maonesho yenu kuwa hata walimu wenye mahitaji maalumu wanaweza kutumia maktaba mtandao na mfumo wa kidijitali haya ni mapinduzi makubwa katika kipindi hiki cha miaka 50”
Kwa Upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amempongeza Rais Dk. Samia kwa mageuzi makubwa aliyoyafanya katika sekta ya elimu nchini “Ni kazi kubwa sana imefanyika katika kuandaa mitaala mipya, wakati Serikali ilipokuwa inazindua Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la Mwaka 2023 tulikuwa tunatekeleza maono yake”

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania Dk. Aneth Komba amesema kuwa katika kipindi cha miaka 50, Serikali kupitia TET imefanikiwa kuongeza hazina ya vitabu vya ziada, rejea, Riwaya, Hadithi, ushairi na aina nyingine ya uandishi bunifu pamoja na moduli na maudhui ya kielektroniki yanayolenga kuwaongezea maarifa wanafunzi kwa kutathmini vitabu vya ziada aina 1446 vinavyoandikwa na wachapishaji binafsi.