Home KITAIFA Rais Dk.Samia azindua Hospitali ya zaidi ya shilingi bilioni 4,Wananchi wampa tano

Rais Dk.Samia azindua Hospitali ya zaidi ya shilingi bilioni 4,Wananchi wampa tano

Simiyu

RAIS Dk.Samia Suluhu Hassan leo Juni, 17 2025 amezindua Hospitali ya Wilaya ya Itilima iliyogharimu shilingi bilioni 4.7 iliyojumuisha ujenzi wa miundombinu na ununuzi wa vifaatiba huku wananchi wakimpongezi.

Rais amezindua Hospitali hiyo leo akiwa kwenye siku ya tatu ya ziara yake ya kikazi katika mkoa wa Simiyu ambapo tangu aanze ziara hiyo amekagua na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo iliyogharimu mabilioni ya fedha huku akifanya mikutano na wananchi.

Akizungumza mara baada ya kuzindua hospitali hiyo, amefafanua kuwa dhamira ya Serikali yake ni kusogeza huduma bora kwa wananchi.

” Nimeridhishwa na miundombinu ya hospitali hii ilivyo ya kisasa na fedha iliyotumika, kimsingi hospitali hii ina kila kitu ambacho kinatakiwa kuwepo kwenye hospitali”. Ameongeza Rais huku akishangiliwa na wananchi waliofurika kumlaki.

Aidha, ameeleza kuwa Serikali imejenga hospitali kama hiyo katika maeneo tofauti ya nchi lengo likiwa ni kuwapunguzia wananchi kwenda umbali mkubwa kupata huduma za afya.

Amewaahidi wananchi kuwa Serikali yake itaendelea kuwaletea maendeleo wananchi wake na kuwa kuwaboreshea maisha.

Awali akimkaribisha Rais Samia ili aongee na maelfu ya wananchi katika mkutano wa kuhitimisha ziara kwa siku ya leo Waziri wa Ardhi, nyumba na maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi kwaniaba ya Waziri wa Nchi, TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa amesema TAMISEMI kupitia Idara ya afya ilipewa shilingi trilioni 1.34 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali za wilaya na zahanati nchini nzima kwenye Halmashauri zote 184 zikihusisha pia ununuzi wa Vifaa tiba.

Aidha ameongeza kuwa Rais Samia ameongeza bajeti ya ujenzi wa barabara za mijini na vijijini katika Halmashauri ya Wilaya ya Itilima kutoka Shilingi Milioni 800 mwaka 2021 hadi kufikia Bilioni 2.5, suala ambalo limewezesha barabara zote za wilaya hiyo kupitika kwa msimu wote wa mwaka.

Anna Masanja, Mkazi wa Itilima amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia imefanya maboresho makubwa kwenye kila sekta katika kipindi kifupi cha uongozi wake.

“Kwa kusema ukweli Mama Samia ametuheshimisha wananchi kwa kufanya makubwa kwenye elimu, miundombinu, afya, umeme hata maji” ameongeza Buliga Amos Mkazi wa Meatu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here