Home SIASA Kaeni kimya kama hamjui nchi ilikotoka-Wasira

Kaeni kimya kama hamjui nchi ilikotoka-Wasira

Na Mndishi Wetu, Geita

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira amesema tangu kupata uhuru Tanzania imepata maendeleo makubwa na kwamba wanaosema hakuna kilichofanyika ni vema wakakaa kimya, wasiwe na tabia ya kasuku kukariri wasiyoyajua.

Wasira ameyasema hayo Juni 17, 2025 alipokuwa akizingumza katika mkutano wa hadhara Katoro, mkoani Geita akiwa katika ziara ya kukagua uhai wa Chama na kuzungumza na wananchi.

Akieleza kuhusu maendeleo yaliyofanyika nchini tangu kupatikana kwa uhuru alisema ni makubwa na wenye umri mkubwa wanajua vizuri nchi ilivyokuwa na wamekuwa wakishuhudia hatua mbalimbali zinazofanywa na serikali inayoundwa na CCM.

“Labda ninyi vijana hamwelewi lakini niwaambie wakoloni wa Kijerumani na wakoloni wa Kiingereza wamekaa Tanganyika miaka 75, Wajerumani wamekaa miaka 35, wamejenga reli kwa viboko bila malipo.

Waingereza wamekaa miaka 40 walitumwa na Umoja wa Mataifa (UN) watuendeleze tujitawalie, lakini miaka 40 ya Waingereza wametuacha na wahandisi wawili katika nchi isiyo na barabara,”‘amesema.

Amefafanua kuwa Wameachia nchi hakuna daktari hata mmoja walikuwepo madaktari kutoka India na Pakistani nao walikuwa Dar es Salaam. Wakati wanapata uhuru wakina mama walikuwa hawajifungui ila wanazaa maana hakukua na kliniki, hivyo walikuwa wanazaa kama ng’ombe anavyozaa ndama.

Amesema umeona wapi ng’ombe ana kliniki (ya uzazi)? Hiyo ndio hali waliyotuacha nayo (wakoloni) wametuacha hatuna barabara.

“Leo anakuja mtu hajafikisha umri wa miaka 30 au miaka 40 anawaambia hakuna maendeleo. Wewe uliwahi kutembea kwa miguu, kuna maendeleo, hao wanaosema hakuna maendeleo ambayo yamefanyika akija muulizeni hivi kwako maendeleo ni kitu gani?,” amesema.


Wasira amesema inawezakana wanaosema hakuna kilichofanyika anazungumza kama kasuku, maana kasuku huwa anakariri tu haelewi hata maana ya maneno anayosema na hao ndio wanasiasa wapya, wao wamejitawala walikuwa na msomi mmoja tu mwenye ‘Master’ (shahada ya uzamili) Julius Nyerere ndio alikuwa ameandaliwa na Wakoloni kwa miaka 75.

“Leo wala sio Tanganyika nilikuwa namuuliza Mkurugenzi wa Bukombe asubuhi anasema ana wahandisi 12, nikasema wewe ni tajiri kuliko Tanganyika ya mwaka 1970 maana kulikuwa na wahandisi wawili wewe unao 12. Namuuliza madaktari anasema wengi tu sisi hatukuwa na daktari.

Hii ndio nchi tuliyorithi, leo unaweza kwenda mkoa wowote wa Tanzania kwa lami. Zamani wakati tunakabidhiwa nchi lami ilikuwa inatoka Dar es Salaam mpaka Morogoro kwa sababu kulikuwa na wazungu wanalima mkonge, ilikuwa inatoka Tanga mpaka Korogwe kwa sababu kulikuwa na wazungu wanalima konge,” amesema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here