Na Abdallah Nassoro- Morogoro
TAASISI ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) inashiriki katika maadhimisho ya miaka 20 ya Chuo Kikuu cha Waislam (MUM), ambapo madaktari Bingwa na wabobezi wanatoa huduma ya ushauri na matibabu kwa wananchi wa mji wa Morogoro na viunga vyake.

Matibabu hayo yameanza kutolewa leo Juni 18, 2025 katika viwanja vya chuo hicho na yataendelea hadi Juni 20, 2025.
Daktari Bingwa wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya fahamu MOI, Dk. Zarina Shabhay amesema ushiriki wa MOI katika maadhimisho hayo yamelenga kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi.
“Wananchi wamepata fursa ya kupata matibabu ya kibingwa na kibobezi ya Mifupa, Ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu bure na karibu yao, kama si kusogeza huduma hizi karibu yao wangelazimika kusafiri hadi jijini Dar es Salaam,” amesema Dk. Zarina na kuongeza kuwa

“Ni fursa adhimu kwao, hivyo hawana budi kuitumia vizuri kwa kujitokeza kwa wingi kupata matibabu haya ya bure…kwetu MOI ni faraja kuwa hapa na kuungana na wanachuo katika maadhimisho haya”
Taasisi ya MOI imekuwa na utaratibu wa kusogeza huduma karibu na wananchi ili kuwapunguzia gharama za kusafiri umbali mrefu kumfuata huduma hizo.