Moscow, Russia
Rais wa Urusi, Vladimir Putin, hana mpango wowote wa kuzungumza na mwenzake wa Marekani, Donald Trump, kufuatia mashambulizi ya kijeshi ya Marekani dhidi ya maeneo ya nyuklia ya Iran, kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu ya Kremlin iliyotolewa Jumapili na kuripotiwa na shirika la habari la serikali la TASS.
Hata hivyo, Kremlin imeongeza kuwa endapo kutahitajika, mazungumzo kati ya viongozi hao wawili yanaweza kupangwa kwa haraka.
Urusi na Iran zilisaini mkataba wa ushirikiano wa kina mwezi Januari mwaka huu, hatua iliyodhihirisha uhusiano wa karibu na wa kimkakati kati ya mataifa hayo mawili. Hata hivyo, mkataba huo haukuweka masharti ya nchi moja kuitetea nyingine endapo itashambuliwa.
Wakati huo huo, katika mazungumzo ya simu yaliyofanyika Alhamisi, Rais Putin na Kiongozi wa China, Xi Jinping, walilaani vikali mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran, kwa mujibu wa taarifa kutoka Kremlin na Wizara ya Mambo ya Nje ya China.
Ingawa taarifa hizo hazikutaja moja kwa moja jukumu la Marekani, Rais Xi alitoa ujumbe ulioonekana kumlenga Trump, akisisitiza kuwa “mataifa yenye ushawishi mkubwa” katika mzozo huo yanapaswa kusaidia kutuliza hali badala ya kuichochea.