Mwandishi wetu, Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika Serikali ya Awamu ya Nane katika nyanja mbalimbali yanatokana na mchango mkubwa wa Mhimili wa Baraza la Wawakilishi.

Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo katika hafla ya kuwapongeza na kuwaaga Wajumbe wa Baraza la Kumi la Wawakilishi, iliyofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip, Uwanja wa Ndege, Mkoa wa Mjini Magharibi Juni,23 2025.

Ameeleza kuwa anauthamini mchango mkubwa uliotolewa na Mhimili huo wa Baraza la Wawakilishi katika kujenga nchi.
Amefafanua kuwa utekelezaji bora wa kazi za mihimili ya nchi ambayo ni Mahakama, Serikali na Baraza la Wawakilishi umekuwa na mchango mkubwa katika kufanikisha majukumu ya kuwahudumia wananchi.

“Umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na Baraza la Wawakilishi unaongeza uwajibikaji kwa kuwepo kwa usimamizi na ufuatiliaji mzuri wa Serikalini,” amesema.
Pia ametumia fursa hiyo kuwasisitiza Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu kwa kupiga kura, na kila mwenye sifa na haki ya kushiriki uchaguzi kufanya hivyo.

Rais Dkt. Mwinyi amewaaga na kuwatakia kila la heri Wajumbe wa Baraza la Kumi la Wawakilishi, ambao wameagwa rasmi baada ya Rais kutangaza kuwa atalivunja Baraza hilo ifikapo Agosti,13 2025, mara baada ya kumaliza kipindi cha miaka mitano kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar.

Baraza la Wawakilishi limemtunuku Rais Dk. Mwinyi Tuzo Maalum kwa kuthamini na kutambua mchango wake mkubwa kwa Baraza hilo, sambamba na uongozi wake unaoleta mageuzi katika sekta mbalimbali za maendeleo.