Home KITAIFA Rais Mwinyi: Mafanikio ya Serikali yamechangiwa na Baraza la Wawakilishi

Rais Mwinyi: Mafanikio ya Serikali yamechangiwa na Baraza la Wawakilishi

Na Mwandishi Wetu – Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema mafanikio yaliyopatikana katika Serikali ya Awamu ya Nane yametokana na mchango mkubwa wa Baraza la Wawakilishi katika kutekeleza majukumu yake kwa weledi na uwajibikaji.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo Juni 23, 2025, katika hafla ya kuwaaga na kuwapongeza Wajumbe wa Baraza la Kumi la Wawakilishi, iliyofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip, Uwanja wa Ndege, Mkoa wa Mjini Magharibi.

“Mafanikio tuliyoyapata katika nyanja mbalimbali ni matokeo ya ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na Baraza la Wawakilishi. Nawapongeza kwa kazi kubwa mliyoifanya katika kusimamia maendeleo ya Zanzibar,” alisema Rais Mwinyi.

Aidha, alieleza kuwa utekelezaji wa majukumu ya mihimili mitatu ya dola – Serikali, Mahakama na Baraza la Wawakilishi – umewezesha kupatikana kwa huduma bora kwa wananchi, huku akisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali na Baraza hilo umeimarisha uwajibikaji serikalini kupitia usimamizi na ufuatiliaji madhubuti wa miradi ya maendeleo.

Katika hafla hiyo, Rais Mwinyi alitoa wito kwa Wajumbe hao kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu ujao kwa kutumia haki yao ya kupiga kura na kuhamasisha wananchi kufanya hivyo kwa amani.

Rais Mwinyi pia alitangaza kuwa Baraza la Kumi la Wawakilishi litavunjwa rasmi Agosti 13, 2025, baada ya kukamilika kwa kipindi cha miaka mitano kama inavyoelekezwa na Katiba ya Zanzibar.

Kwa kutambua mchango wake katika kuimarisha taasisi hiyo ya kidemokrasia, Baraza la Wawakilishi lilimtunuku Rais Mwinyi Tuzo Maalum, ikiwa ni ishara ya kuthamini uongozi wake uliosheheni mageuzi katika sekta mbalimbali za maendeleo visiwani humo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here