Na Mwandishi Wetu, Lajiji
Klabu ya Simba haikuhudhuria mkutano wa kabla ya mchezo (Pre-Match Conference) uliopangwa kufanyika leo Juni 24, 2025 saa 5:30 asubuhi, jijini Dar es Salaam, hatua iliyolazimu Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara kuahirisha mkutano huo rasmi.
Mkutano huo, ambao ni sehemu ya maandalizi ya mchezo muhimu wa Ligi Kuu utakaopigwa kesho Juni 25, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, uliandaliwa na Bodi ya Ligi kwa mujibu wa kanuni na utaratibu wa mashindano.
Akizungumza na waandishi wa habari, Afisa Habari wa Bodi hiyo, Karimu Boimanda, alisema kuwa walifanya jitihada mbalimbali kuwasiliana na uongozi wa Simba SC lakini hawakufanikiwa.
“Tumefanya jitihada zote, lakini hadi sasa hatujawapata. Kwa kuwa hili ni suala la kikanuni na kuna ratiba nyingine za kimchezo, tunatangaza rasmi kuwa mkutano umeahirishwa. Taarifa zaidi zitatolewa baadaye,” alisema Boimanda.
Aidha, Boimanda alibainisha kuwa Bodi itaendelea kufuatilia ili kubaini sababu ya kutohudhuria kwa wawakilishi wa Simba na hatua zaidi zinaweza kuchukuliwa baada ya tathmini ya kina kufanyika.
Kutohudhuria kwa Simba katika mkutano huo kumezua maswali miongoni mwa wadau wa soka, hasa ikizingatiwa kuwa mechi hiyo ni ya muhimu kwa msimamo wa ligi.
