Home KITAIFA Rais Dk.Mwinyi awatunuku Kamisheni Maafisa wapya 164 Mkupuo wa 06

Rais Dk.Mwinyi awatunuku Kamisheni Maafisa wapya 164 Mkupuo wa 06

Na Mwandishi wetu, Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, ambaye pia ni Kamanda Mkuu wa Idara Maalum za SMZ, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewatunuku Kamisheni Maafisa wapya 164 Mkupuo wa 06 kwa mwaka 2024-2025 wa Idara Maalum za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Akizungumza na Maafisa hao wakati wa hafla ya kufunga kozi hiyo, amewasisitiza kuyatumia mafunzo na elimu waliyoipata ili kuleta mabadiliko chanya na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao katika maeneo ya kazi.

Hafla hiyo imefanyika leo Juni, 26 2025 katika Chuo cha Uongozi cha Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU), Dunga, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja, Maafisa hao ni kutoka Jeshi la Kujenga Uchumi na Kikosi cha Valantia.

“Serikali itaendelea kuziamini idara maalum za SMZ kwa ajili ya ulinzi wa nchi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hivyo itaendelea kuimarisha maslahi ya wapiganaji hawa ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa weledi na bidii kwa lengo la kuchangia maendeleo ya nchi,” amesema Dk.Mwinyi.

Amewasisitiza maafisa hao kudhihirisha elimu na mafunzo waliyoyapata kwa vitendo ili kuleta mabadiliko chanya, kuongeza ufanisi, na kuzingatia sheria na miongozo ya kudumu ya Idara za SMZ.

Vilevile, amesema kuwa Serikali inakusudia kukifanya chuo hicho kuwa cha kimataifa na kitovu cha kuandaa Maafisa wa Idara Maalum za SMZ wenye weledi na uadilifu.

Kwa upande mwingine, Rais Dkt. Mwinyi pia amelipongeza Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa ushirikiano wake katika kufanikisha mafunzo ya Maofisa hao, na kusisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano huo wakati wote.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here