Home KITAIFA Wizara ya Nishati tembeeni kifua mbele mnafanya kazi nzuri-Dk. Biteko

Wizara ya Nishati tembeeni kifua mbele mnafanya kazi nzuri-Dk. Biteko

📌Asema Nishati ni Sekta inayokua kwa kasi; anajivunia kufanya nayo kazi

📌Asema Rais Samia amekuwa mstari wa mbele kuiwezesha Sekta kusonga mbele

📌 Afunga rasmi Nishati Bonanza 2025

📌 TANESCO, TPDC zang’ara michezo ya Wavu Kikapu na Kamba

📌 Wakuu wa Taasisi waipongeza Wizara ya Nishati kuandaa Bonanza lililofana

📌Mbio za wenye umri mkubwa zawa kivutio Nishati Bonanza

Na Mwandishi wetu, Dodoma

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk. Doto Biteko amesema Sekta ya Nishati ni miongoni mwa sekta zinazotajwa kukua kwa kasi ya asilimia 14.7 ukiacha ile ya Sanaa na Burudani inayokua kwa asilimia 17 na hivyo kuwa miongoni mwa sekta zinazofanya vizuri hapa nchini.

Dk. Biteko ameyasema hayo leo Juni 28, 2025 wakati akifunga Bonanza la Nishati kwa mwaka 2025 ambalo ameliasisi likishirikisha Wizara ya Nishati na taasidi zilizo chini ya Wizara ya Nishati.

‘’ Ndugu zangu nipende kuwapongeza sana Wizara na taasisi zake kwa kazi nzuri na kubwa mnayoifanya kuwahudumia Watanzania na mimi kama kiongozi wenu najivunia sana kufanya kazi na Wizara hii na kama kuna mahali najivunia ni ufanyaji kazi wenu kama Wizara chini ya Katibu Mkuu Mha . Felchesmi Mramba,” amesema Dk.Biteko

Amesema Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele kuiwezesha sekta ya nishati kufanya vizuri kwa kutenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ambapo amewaasa Watendaji kutembea kifua mbele kwani kazi wanayofanya ni njema na imeleta matokeo chanya kwa wananchi hususani kusambaza umeme vijijini na kuongeza kuwa, Tanzania imekuwa mfano kwa nchi nyingine Afrika kutekeleza mpango wa misheni 300 wa kupeleka umeme Waafrika milioni 300 ifikapo 2030.

Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema Bonanza la mwaka huu limekuwa na ongezeko la idadi ya washiriki kutokana na mwamko wa taasisi chini ya Wizara ya Nishati kuleta watu wengi zaidi ikilinganishwa na mwaka jana ambapo mwaka huu idadi ya washiriki imefikia watu 1000.

Amesema Bonanza hilo lilikuwa na kaulimbiu, Michezo kwa Afya Bora, Shiriki Uchaguzi 2025.

Katika bonanza hilo michezo Mbalimbali ilishindaniwa ikiwemo mpira wa miguu, pete, wavu, kikapu, kuvuta kamba, kupenya kwenye pipa, kukimbia na yai mdomoni, karata, bao, drafti.

Mshindi wa mpira wa kikapu kwa Wanaume na wanawake alikuwa ni TANESCO, na kwa upande wa mpira wa wavu wanawake na wanaume TANESCO pia imeibuka kidedea.

Kwa upande wa mpira wa Miguu mshindi wa kwanza ni TANESCO na wa pili ni TPDC. Kwa upande wa mpira wa kamba wanaume mshindi wa kwanza ni TPDC akifuatiwa na TANESCO, kwa upande wa wanawake kamba mshindi wa kwanza ni TPDC na wa pili ni EWURA.

Katika hatua nyingine, Wizara ya Nishati kupitia Katibu Mkuu, Mha. Felchesmi Mramba amemkabidhi Naibu waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt Doto Biteko Tuzo maalumu kwa kutambua mchango wake kwenye sekta ya Nishati na kwa kuwa muasisi wa Nishati Bonanza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here