Home UCHUMI Riba ya Benki Kuu yapungua kutoka asilimia 6 hada 5.75

Riba ya Benki Kuu yapungua kutoka asilimia 6 hada 5.75

Na Esther Mnyika, Dar es Salaam

KAMATI ya Sera ya Fedha Benki Kuu ya Tanzania(BoT) imeamua kushusha  kiwango cha riba ya  benki hiyo katika robo  ya tatu ya mwaka kwa asilimia 5.75  kutoka asilimia sita  iliyodumu kwa robo mbili za mwaka huu.

Riba hiyo imetangazwa leo Julai, 3 2025 jijini Dar es Salaam na Gavana wa BoT, Emmanuel  Tutuba, jijnini na kusema itaanza kutumika  kuanzia Julai hadi Septemba, mwaka huu.

“Katika kikao chake kilichofanyika jana (juzi),Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) iliamua kupunguza Riba ya Benki Kuu kutoka asilimia  sita hadi asilimia 5.75 hivyo Benki Kuu itatekeleza sera ya fedha kuhakikisha riba ya mikopo ya siku saba baina ya benki inabaki ndani ya wigo wa asilimia 3.75 hadi 7.75,” ameseama.

Gavana Tutuba amesema uamuzi huu unaakisi imani ya kamati katika mwenendo wa mfumuko wa bei ambao umeendelea kubaki ndani ya wigo wa asilimia tatu hadi tano na matarajio yanayoonesha kuendelea kuwa tulivu ndani ya wigo huo.

“Hali hii inatokana na utekelezaji madhubuti wa sera za fedha na bajeti, kuanza kwa msimu wa mavuno, pamoja na utulivu wa thamani ya shilingi ya Tanzania.

“Ingawa migogoro ya kisiasa duniani na ongezeko la ushuru wa bidhaa za forodha umeongeza sintofahamu katika mwenendo wa uchumi wa dunia, mazungumzo na makubaliano ya hivi karibuni yanaashiria hatari hizi zinaweza kupungua,” ameseama.

TATHMINI MWENENDO WA UCHUMI

Kamati hiyo ilipitia mwenendo wa uchumi wa ndani na kubaini kuwa umeendelea kuimarika kwa kasi ya kuridhisha, ukichochewa na uwekezaji mkubwa wa serikali katika miundombinu na kuongezeka kwa shughuli za sekta binafsi, kutokana na kuimarika kwa mazingira ya ufanyaji biashara.

Gavana Tutuba amesema tathmini ya Kamati ya mwenendo wa uchumi wa dunia na matarajio ya baadaye, inabaini kuongezeka kwa hali ya sintofahamu katika mwenendo wa uchumi na biashara duniani.

Amesema hali hiyo inatokana na kuongezeka kwa migogoro ya kisiasa duniani na ushuru wa forodha na pia imechangia kudhoofisha matarajio ya ukuaji wa uchumi wa dunia kwa mwaka huu.

 Amesema  ukuaji wa uchumi kwa robo ya pili ya mwaka huu, ulikuwa na mwenendo tofauti baina ya nchi, huku nchi chache tu duniani zikiimarika kiuchumi.

KUPUNGUA KWA MFUMUKO WA BEI

Tutuba amesema mfumuko wa bei umepungua katika nchi nyingi, kutokana na utekelezaji wa sera ya fedha inayopunguza ukwasi katika kipindi cha nyuma na kushuka kwa bei za chakula na nishati.

“Mfumuko wa bei unatarajiwa kuendelea kushuka, ingawa kwa kasi ndogo kuliko ilivyotarajiwa awali, kutokana na kutotabirika kwa sera za uchumi na biashara duniani.

“Bei za bidhaa katika soko la dunia zilikuwa na mwenendo tofauti. Bei ya dhahabu iliongezeka hadi kufikia dola za Marekani 3,282.40 mwishoni mwa Juni, mwaka huu, kutoka dola za marekani 2,855.73 mwishoni mwa Machi, mwaka huu,” amesema.

Amesema hilo linatokana na  kuongezeka kwa migogoro ya kisiasa na mivutano ya kibiashara duniani, ambayo imesababisha ongezeko la mahitaji ya dhahabu kama rasilimali salama ya uwekezaji na kuweka akiba.

 Katika hatua nyingine, bei ya mafuta ghafi ilipungua hadi dola za marekani 65.92 kwa pipa kutoka dola za marekani 74.35, kutokana na kupungua kwa mahitaji duniani  na kuongezeka kwa usambazaji kutoka nchi wanachama wa OPEC+.

Tutuba amesema benki kuu nyingi duniani zinatarajiwa kutekeleza kwa umakini sera za fedha,huku zikijaribu kudhibiti hatari zinazoweza kuongeza mfumuko wa bei na kuendelea kuchochea ukuaji wa uchumi.

“Uchumi wa ndani uliendelea kuwa stahimilivu na unatarajiwa kuendelea kuimarika, ukuaji wa uchumi kwa Tanzania Bara unakadiriwa kufikia asilimia 5.8 katika robo ya kwanza na asilimia 5.5 katika robo ya pili ya mwaka huu.

“Ukuaji huu umechangiwa zaidi na sekta za kilimo, ujenzi na huduma za fedha na bima, hivyo basi uchumi wa ndani unatarajiwa kuendelea kuimarika, ambapo ukuaji wake unatarajiwa kufikia asilimia 6.0 na 6.9 katika robo ya tatu na ya nne, mtawalia,” amesema.

UCHUMI WA ZANZIBAR

Tutuba amesema uchumi wa  Zanzibar unatarajiwa kufuata mwelekeo huo huku kasi hiyo ya ukuaji inachochewa na uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya reli, barabara, viwanja vya ndege, na viwanja vya michezo kwa ajili ya maandalizi ya mashindano ya CHAN na AFCON.

Amesema na uwekezaji unaoendelea katika sekta za kilimo na madini. Matarajio haya chanya yanathibitishwa na matokeo ya tafiti za Mtazamo wa Masoko na Maoni ya Watendaji Wakuu wa Kampuni zilizofanyika Mei, mwaka huu. 

Pia Tutuba  amesema mfumuko wa bei  kwa Tanzania Bara ulikuwa wastani wa asilimia 3.2 katika robo ya pili ya mwaka 2025, ukiakisi utekelezaji madhubuti wa sera ya fedha na utulivu wa bei za bidhaa zisizo za chakula na zile za nishati.

Mfumuko wa bei za chakula uliongezeka kidogo, kutokana na changamoto za usafirishaji zilizosababishwa na mvua kubwa katika baadhi ya maeneo.

Kwa upande wa Zanzibar, mfumuko wa bei ulipungua hadi asilimia 4.2, Mei mwaka huu, kutoka asilimia 5.3 mwaka mmoja uliopita, hali iliyochangiwa zaidi na kushuka kwa bei za chakula.

Vilevile ujazi wa fedha uliendelea kuongezeka kwa kasi ya kuridhisha, ukiakisi ongezeko la mahitaji ya shughuli za kiuchumi.

“Ujazi wa fedha ulikua kwa wastani wa asilimia 19.1 kwa mwaka katika robo ya pili ya mwaka huu, ikilinganishwa na asilimia 15.4 katika robo ya kwanza. Ukuaji huu ulitokana kwa kiasi kikubwa na ongezeko la mikopo kwa sekta binafsi, iliyokua kwa asilimia 16.7, ikiashiria kuimarika kwa upatikanaji wa mitaji na mazingira ya biashara.

SEKTA YA FEDHA NI IMARA

 Gavana Tutuba amesema sekta ya fedha iliendelea kuwa imara na thabiti na sekta ya benki imeendelea kuwa na mtaji na ukwasi wa kutosha na yenye kutengeneza faida.

“Ukuaji wa amana na utoaji mikopo ulichangiwa na kuongezeka kwa mtandao wa huduma za mawakala wa benki na matumizi ya mifumo ya kidijitali katika utoaji wa huduma. Uwiano wa mikopo chechefu ulipungua hadi asilimia 3.4 Mei, mwaka huu ukiwa chini ya kiwango cha juu kinachovumilika cha asilimia tano,”amesema.

Amesema mwenendo huu unaashiria kuongezeka kwa ubora wa mikopo na kuimarika kwa usimamizi madhubuti wa vihatarishi katika sekta ya benki.

Tutuba amesema utekelezaji wa sera ya bajeti kwa Tanzania Bara na Zanzibar ulichangia kufikia malengo ya utekelezaji wa sera ya fedha.  Makusanyo ya mapato yalifikia malengo yaliyowekwa, yakichangiwa na uboreshaji wa usimamizi wa kodi na kuongezeka kwa ulipaji kodi kwa hiari.

“Matumizi yaliendana na rasilimali zilizopo, jambo linalioashiria umakini wa serikali katika utekelezaji wa bajeti. Kamati ya Sera ya Fedha ilibaini kuwa utekelezaji madhubuti wa sera ya bajeti na maboresho yanayofanyika, yatachangia ukuaji endelevu wa uchumi na kusaidia sera ya fedha katika kuhakikisha mfumuko wa bei unakuwa mdogo na tulivu,” amesema.

Pia, deni la serikali liliendelea kuwa himilivu, ndani ya viwango vinavyokubalika kimataifa.

KUIMARIKA SEKTA ZA NJE

Tutuba amesema sekta ya nje imeendelea kuimarika katika robo ya pili ya mwaka huu ambapo nakisi ya urari wa malipo ya kawaida ilikadiriwa kupungua hadi kufikia dola za Marekani milioni 797.1 katika robo ya pili ya mwaka huu, kutoka dola za Marekani milioni 872.1 katika robo ya pili ya mwaka uliopita.

“Katika mwaka 2024/2025, nakisi ya urari wa malipo ya kawaida unakadiriwa kuwa asilimia 2.6 ya Pato la Taifa (GDP), ikipungua kutoka asilimia 3.7 mwaka uliotangulia, ikichangiwa na ongezeko la mauzo ya bidhaa nje ya nchi ikiwemo, dhahabu, utalii, mauzo ya bidhaa za viwandani na mazao ya biashara,” amesema.

 Amesema kwa upande wa Zanzibar, urari wa malipo ya kawaida unakadiria kufikia ziada ya dola milioni 611.1 kwa mwaka 2024/2025, ikilinganishwa na ziada ya dola milioni 428.5 mwaka uliopita, ukichangiwa na ongezeko la mapato yatokanayo na shughuli za utalii.

Pia akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuwa ya kutosha, ikikadiriwa kufikia takribani dola za marekani bilioni sita, ikiwa ni kiwango cha juu kufikiwa kwa hivi karibuni.

“Akiba hii inatosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kwa takribani miezi 4.8. Sekta ya nje inatarajiwa kuendelea kuimarika tunapoelekea kwenye msimu wa mauzo ya bidhaa na huduma, hususan utalii, mazao ya biashara na dhahabu,” amesema.

SHULINGI YA TANZANIA NI TULIVU

Tutuba alisema shilingi ya Tanzania imeendelea kuwa tulivu dhidi ya sarafu nyingi za kigeni.

“Thamani ya shillingi dhidi ya dola ya Marekani ilishuka kwa kasi ndogo ya asilimia 0.2 kwa mwaka ulioishia Juni, mwaka huu, ikilinganishwa na kushuka kwa asilimia 12.5 katika kipindi kama hicho mwaka jana.

“Utulivu huu umechangiwa na kuongezeka kwa ukwasi wa fedha za kigeni kutokana na mapato ya utalii, na mauzo  ya bidhaa nje ya nchi, hususan dhahabu na tumbaku,”amesema.

Pia, utekelezaji madhubuti wa sera ya fedha na usimamizi wa kanuni zinazotaka miamala ya fedha ya ndani ya nchi kufanyika kwa shilingi vimechangia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha utulivu wa shillingi.

Vilevile, ongezeko la ununuzi wa dhahabu kutoka ndani ya nchi kwa ajili ya kuongeza akiba ya fedha za kigeni lilichangia kuongeza imani kwa sarafu ya Tanzania.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here