Na Mwandishi wetu, Iringa
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameziagiza Mamlaka za Mikoa na Wilaya kufanya kaguzi za mara kwa mara katika maeneo yaliyohifadhiwa, vyanzo vya maji na mito ili kudhibiti vitendo vya uharibifu wa mazingira.

Ametoa agizo hilo leo Jumamosi Julai 5, 2025 aliposhiriki katika mbio za Great Ruaha Marathon (GRUMA 2025) zilizoanzia na kuishia kwenye eneo la Ibuguziwa, ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, mkoani Iringa.
“Wekeni utaratibu mzuri wa matumizi ya vyanzo hivyo, tunataka kuona mikondo yote ya maji inayokwenda kulisha mto mkuu, inahifadhiwa ili tupate maji mengi na yaweze kuchangia kwenye shughuli za kimaendeleo, mto Ruaha Mkuu unapeleka maji katika bwawa letu la kuzalisha umeme la Mwalimu Nyerere,”amesema.
Majaliwa ameziagiza mamlaka hizo zibainishe vyanzo muhimu vya maji vilivyopo kwenye maeneo yao na kuweka utaratibu maalum na wawazi juu ya namna ya kuhifadhi vyanzo hivyo ili viweze kuzalisha maji ya kutosha. “Mimi ninawasihi wekeni Sheria ndogo zinazodhibiti uharibifu na kutambua vyanzo hivyo ni muhimu katika maeneo yenu”.

Waziri Mkuu ameagiza kusimamiwa kwa mipango ya matumizi bora ya ardhi kuanzia ngazi ya vijiji. “Sambamba na kuhakikisha elimu ya uhifadhi, upandaji miti na ajenda ya utunzaji wa mazingira inakuwa ya kudumu kuanzia vitongojini mpaka vijijini”
Pia, Majaliwa amempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuhakikisha anaisimamia sekta ya utalii ili iweze kuwa na tija na kuchangia katika pato la Taifa.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Heri James amempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia utekelezaji wa ahadi zake zinazolenga kukuza sekta ya utalii katika ukanda wa kusini. “Baadhi ya mambo ambayo anayafanya na ni ishara ya kukuza utalii nk pamoja na kukamilisha uwanja wa ndege wa Iringa, ujenzi wa barabara kutoka Iringa hadi Msembe, ujenzi hosteli za wageni ndani na nje ya hifadhi, ama kwa hakika ameamua kuongeza hadhi ya utalii kwenye ukanda huu.”
Naye, Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), CPA (T) Musa Nassoro Kuji, amesema kuwa ujio wa The Great Ruaha Marathon umekuwa baraka kubwa katika sekta ya utalii ambapo imesaidia kufungua utalii kwa ukanda wa kusini.

“Tunataka kuona marathon hii iwe kubwa na ya kimataifa, tangu tumeanza marathon hii imesaidia kuongeza idadi ya watalii kwenye ukanda wa kusini, tunataka watalii waje na dunia itutambue kupitia marathon hii,”amesema.
Aidha, ameongeza kuwa Shirika hilo litaendelea kutunza maliasili zilizopo nchini ili kuvirithisha kwa vijazi vijavyo.

Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP), Shigeki Komatsubara amesema kuwa hizi sio mbio tu bali ni harakati za kulinda mto Ruaha Mkuu ambao ni muhimu kwa ajili ya ustawi wa binadamu, wanyamapori na mfumo mzima wa ikolojia “Leo sio tu tunakimbia kwa ajili ya mazoezi bali kwa uhifadhi na uelewa”