Na Esther Mnyika, Dar es Salaam
MKUFUNZI wa Chuo Kikuu Dodoma (UDOM) kutoka Idara ya Kemia, Dismas Ngoda ameiomba serikali kuendelea kuwekeza kwenye matumizi ya dawa asili ambazo zinapatikana kwa urahisi na mimea inapatikana kwa wingi.

Akizungumza leo Julai, 5 2025 jijini Dar es Salaam na Lajiji Digital kwenye maonesho ya 49 Kimataifa Sabasaba Ndoga amesema dawa za asili zinatengenezwa na Chuo hicho zinatibu magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama sukari, vidonda vya tumbo na maralia.
Amesema kwenye maonesho ya sabasaba mwaka jana walikuja na dawa moja ambayo inatibu ugonjwa wa sukari lakini mwaka huu wameongeza dawa ya asili ambayo inatibu maralia na vidonda vya tumbo kutokana na mahitaji ya watu.
“Wananchi wanatakiwa kutumia dawa za asili kutoka kwenye za taasisi ambazo zimepewa usajili rasmi na zinazotambulika kisheria,” amesema Ndoga.
Amesema muunganiko wa dawa hizo wamezingatia Mchanganyiko wa viambata mbalimbali kwa lengo la kupunguza dozi na upunguzaji huo unasaidia kuondokana na changamoto ya magonjwa ya figo,ini, miguu kuvimba na mengineyo.
Amesema dawa za asili zimekuwa na athari ndogo kwa watumiaji ukilinganisha na dawa za viwandani “synthetic medicine”.
Ndoga ameeleza kuwa faida za kutumia dawa za asili dozi zake ni ndogo ikitofautishwa na dawa za Viwanda hivyo kumfanya mgonjwa kumaliza dozi kwa wakati.