Na Esther Mnyika, Dar es Salaam
SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco) limetoa zawadi ya majiko ya umeme kwa Wananchi waliofika katika banda lao lililopo kwenye Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa maarufu sabasaba ili kuhakikisha watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 7,2025 katika viwanja vya maonesho hayo, Mkurugenzi Mtendaji Tanesco, Lazaro Twange amesema wananchi waliofika katika banda lao wamepata fursa ya kupata elimu juu ya umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia na kisha kupatiwa zawadi ya majiko ya umeme.
“Ni maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kwamba watanzania tuhame kwenye kutumia nishati isiyokuwa safi na kutumia iliyosafi, hivyo hapa tunazungumzia nishati ya umeme na tuna majiko haya ya umeme yamefanyiwa utafiti na kuthibitika kuwa yanaweza kupikia na chakula kikaiva kwa kutumia chini ya Unit moja,
“Tunawashukuru watanzania kuja katika banda letu na kwa kuzingatia kuwa wanaelewa tumewashindanisha kwa maswali, aliyeshinda amepata zawadi ya jiko la Umeme, hivyo wakayatumie hayo majiko na wawe mabalozi wazuri kwa wengine,” amesema.

Amesema katika banda la Tanesco kuna majiko hayo ya umeme na wananchi waliojibu vema maswali waliyoulizwa wamepata fursa ya kujishindia zawadi ya majiko hayo kwa ajili ya kuyatumia katika kupikia.
Naye Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO), Sadock Mugendi amesema wamekuwa wakisambaza na kusafirisha umeme maeneo mbalimbali vijijini na kwamba hivi karibuni wamemaliza mradi wa kusafirisha umeme kutoka Tabora mjini kuelekea Katavi wenye kilomita 383 na una msongo wa Kilovolt 132.
“Mradi huu ni mafanikio makubwa kwa Serikali hata hivyo tuna mradi mwingine Mbeya, Katavi yote tunasambaza umeme vijijini, tunaishukuru serikali kuendelea kutuamini kwa kutupatia miradi hii,” amesema.

Kwa upande wake Meneja Mkuu Kampuni ya Uendelezaji Joto Ardhi Tanzania (TGDC), Mathew Mwangomba amesema kwa sasa TGDC katika maeneo ya Mbeya wameanza kuhakiki rasilimali ya joto ardhi na kwamba umeme utakaopatikana utatumiwa katika matumizi ya moja kwa moja na matumizi yatakayoingizwa kwenye Gridi ya Taifa.
“Timu yetu ipo Mbeya eneo ya Mbozi na baada ya kufanya uhakiki tumebaini kuwa eneo hilo lina uwezo wa megawati 70 ambayo tutaingiza katika gridi ya Taifa, TGDC tunawaalika wadau wote wa ndani na nje kuja kuwekeza katika kampuni yetu,” amesema.