📌Asema ni jitihada za uwekezaji uliofanywa na Rais Dk. Samia
📌Aipongeza TANESCO kwa kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amesema hivi sasa Tanzania ina umeme wa kutosha hatua ambayo imechangiwa na kukamilika kwa Miradi mikubwa ya uzalishaji umeme ukiwemo Mradi wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP ) ambao pekee unazalisha Megawati 2115.

Ameyasema hayo leo Julai 10, 2025 Dk. Biteko wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya miradi ya kuzalisha umeme kwa gesi asilia katika vituo vya Kinyerezi I, Kinyerezi I Extension na Kinyerezi II ambapo amesema licha ya kazi kubwa inayofanywa na TANESCO yapo baadhi ya maeneo yalikua na changamoto ya upatikanaji wa umeme lakini mpaka sasa yameendelea kuimarika.
Amefafanua kuwa ili kuhakikisha upatikanaji wa umeme unaendana na mahitaji ya ongezeko la watu TANESCO inatarajia kuongeza uzalishaji umeme katika Kituo cha Kinyerezi III kutoka megawati 600 katika mpango wa awali hadi kufika Megawati 1000 mpango wa sasa.

‘’Nataka niseme mbele yenu ndugu zangu, Rais Samia ndio Kinara wa kufanya haya yote yafanikiwe amefanya uwekezaji mkubwa kwenye Sekta ya Nishati na ndio maana kwenye bajeti iliyopita Wizara hii imepata Shilingi Trilioni 2.3 kikubwa anataka wananchi wapate umeme wa uhakika,’’ amesema Dk. Biteko.
Aidha,Dk.Biteko pia ametumia nafasi hiyo kuipongeza TANESCO kwa maboresho makubwa yanayoendelea kufanyika ya kuwahudumia wateja hasa kwa uharaka wao wa kukabiliana na dharula zozote za umeme zinazojitokeza.

‘’Kuna maboresho makubwa yamefanyika katika kuwahudumia wananchi naona jitihada kubwa zinafanyika, mmekuwa na uharaka wa kushughulikia changamoto za umeme lakini pia niwapongeze kwa kuimarisha Kituo cha miito ya simu sasa wananchi wanahudumiwa bila gharama yoyote,’’ amesisitiza Dk. Biteko.

Katika ziara hiyo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk. Doto Biteko aliongozana na viongozi mbalimbali akiwemo katibu Mkuu wa Wizara ya nishati Mhandisi Felchesmi Mramba, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange.