Home KITAIFA Mume ashikiliwa kwa mauaji ya mkewe

Mume ashikiliwa kwa mauaji ya mkewe

Na Mwandishi wetu, Morogoro

JESHI la Polisi mkoani Morogoro linamshikilia James Lugembe (55), mkazi wa Kitongoji cha Manzese B, Kata ya Mkwatani, Wilaya ya Kilosa, kwa tuhuma za mauaji ya mke wake, Restuta Walela (50).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama, tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Julai 13, 2025, ambapo mtuhumiwa anadaiwa kumkata mkewe kwa kitu chenye ncha kali katika maeneo mbalimbali ya mwili wake na kusababisha kifo chake.

Baada ya tukio hilo, Lugembe alijaribu kujiua kwa kunywa sumu, na kwa sasa amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kilosa chini ya ulinzi wa Polisi.

Kamanda Mkama amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha mauaji hayo ni mgogoro wa kifamilia, ambapo marehemu alikuwa akilalamikia mumewe kushindwa kutekeleza majukumu ya kifamilia, huku mume akimtuhumu mkewe kwa tabia ya ulevi na kuchelewa kurudi nyumbani.

Ameongeza kuwa uchunguzi wa kina unaendelea kwa kushirikiana na wadau wa haki jinai, na mara utakapokamilika, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtuhumiwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here