Na Mwandishi wetu,Dar es Salaam
SERIKALI imeanzisha mafunzo kwa njia ya mtandao ya Afya moja (ECHO) ili kuwajengea uwezo watoa huduma wa kada za afya ya binadamu, wanyama na mazingira kwa ngazi zote.

Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu Dk.Jim Yonazi wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo Julai,15 2025 katika Kituo cha kurushia Mafunzo kwa njia ya mtandao (ECHO HUB) kilichopo katika jengo la Idara ya Utafiti na Mafunzo Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam.
Amesema Serikali inaendelea kukabiliana na majanga na dharula zenye athari kwa afya ya binadamu, wanyama na mazingira hivyo imeona umuhimu wa kuwezesha wataalamu wake kuelewa kwa kina dhana ya Afya Moja.
“Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Wizara za Kisekta na mradi wa USAID Usalama wa Afya Duniani unaotekelezwa na Shirika la CIHEB Tanzania, imeanzisha mafunzo ya mtandao ya Afya moja (ECHO) ili kujenga uwezo kwa watoa huduma wa kada za afya ya binadamu, wanyama na mazingira kwa ngazi zote,”amesema Dk. Yonazi.
Ameongeza kuwa; “Naomba niwahamasishe viongozi na watumishi kutoka sekta mbalimbali kushiriki katika vipindi hivi. Wataalamu wabobezi watawasilisha mada mbalimbali zitakazojenga uwezo wetu katika kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na magonjwa ya mlipuko kwa binadamu na wanyama, visumbufu vya mazao, usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa, usalama wa chakula.

Awali akieleza lengo la uzinduzi wa mafunzo hayo Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Brigedia Generali Ndagala amesema,Mafunzo haya yanayolenga katika kuongeza ufanisi kwa wataalam katika kushughulikia magonjwa ya kizoonotiki, usugu wa vimelea dhidi ya dawa (AMR), hatari za kibailojia, usalama wa chakula na magonjwa yasiyoambukizwa ambayo ni maeneo muhimu yenye changamoto na yanapewa kipaumbele katika Sekta ya Afya nchini Tanzania.
Amefafanua kuwa, Mafunzo haya yatawahusu wataalamu wa Sekta ya Afya moja, Afya, mazingira, mifuko na uvuvi.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Afya na Lishe Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Suzanne Nchalla amesema mpango huo utasaidia watoa huduma ngazi ya msingi kupata uelewa wa Dhana ya Afya Moja na wakati wa utoaji huduma.
Amesema OR- TAMISEMI itashirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu katika kuhakikisha watumishi wa afya ya msingi wanashiriki kikamilifu katika mafunzo hayo.

“Tutawasimamia na kuwakumbusha viongozi wa Halmashauri kuhakikisha wanashiriki vipindi vilivyopangwa ili kupata matokeo chanya na kutimiza azma la mpango huu,”amesema Suzanne.
Naye Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Serikali Dk.Otilia Gowelle amesema Wizara ya Afya inatambua umuhimu wa mashirikiano ya wadau na sekta mbalimbali katika kujiandaa pamoja na kukabiliana na matishio ya mara kwa mara ya magonjwa ya mlipuko pamoja na matukio yenye athari kwa afya ya binadamu.

“Kwa kuzingatia umuhimu wa mafunzo haya, Wizara imekwisha fanya uhamasishaji na itaendelea kuhakikisha wataalam wengi zaidi wanashiriki mafunzo haya wakiwemo wauguzi, madaktari, wafamasia, maafisa afya, wataalam wa maabara na wengineo waliopo katika vituo vya kutolea huduma na maeneo mengine mahsusi,” amesisitiza Dk. Gowelle.
Ameongezea kuwa Wizara ya Afya imekuwa mshiriki na mnufaika mkuu wa ushirikiano uliopo kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano kila inapohitajika.