Na Mwandishi wetu, Dodoma
Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, amezindua rasmi Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 katika hafla iliyofanyika leo Julai,172025 jijini Dodoma, huku akieleza malengo makuu ya kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa kisasa, jumuishi na wenye ushindani wa kimataifa,Katika hotuba yake, Rais Samia ameeleza kuwa dira hiyo inalenga kufanikisha ongezeko la pato la taifa hadi kufikia Dola za Kimarekani trilioni moja na kuongeza kipato cha kila Mtanzania kufikia wastani wa dola 7,000 kwa mwaka ifikapo 2050.

Akizungumza baada ya uzinduzi huo Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara ya TCB, Adam Mihayo, amesema benki hiyo iko tayari kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 iliyozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan jijini Dodoma.
Mihayo amesema TCB inajivunia kuwa sehemu ya mchakato huu mkubwa wa kitaifa, ambao unalenga kuifikisha Tanzania katika uchumi wa kati wa juu na kuongeza pato la taifa hadi kufikia dola trilioni moja za Marekani ifikapo mwaka 2050.

Amesema dira hiyo imeweka malengo makubwa na mwelekeo sahihi wa taifa, huku ikitaja sekta tisa muhimu zitakazoongoza katika maendeleo, zikiwemo sekta za kifedha.
Mihayo alibainisha kuwa ongezeko la watu na mahitaji ya huduma rasmi za kifedha kama bima, teknolojia na huduma za benki vinatoa fursa ya kupanua wigo wa mapato ya serikali kupitia urasimishaji wa uchumi, jambo litakalojenga uwezo mkubwa wa serikali katika kuchochea maendeleo ya wananchi.
“TCB imeanza tayari kuitekeleza dira hiyo kupitia mpango mkakati mpya wa benki ambao umeanza kutekelezwa mwaka jana, kwa kuelekeza nguvu kwenye sekta za uzalishaji badala ya matumizi pekee,anaeleza kuwa benki hii sasa inaelekeza huduma zake kwa wafanyabiashara wa ngazi zote, wakiwemo wadogo, wa kati na wakubwa, hasa kwenye maeneo ya kilimo, ambako zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wamejikita,”amesema.

Kwa mujibu wa Mihayo, TCB pia inasaidia sekta nyingine za kipaumbele kama ujenzi, viwanda, usindikaji wa bidhaa, na kukuza mauzo ya nje. Hatua hizi, amesema, zina lengo la kuhakikisha Tanzania inapata uchumi jumuishi na endelevu kwa wote,amesema dira ya 2050 inaleta matumaini makubwa na ni wajibu wa taasisi za fedha kama TCB kuandaa mazingira bora ya kufanikisha utekelezaji wake.
Amehitimisha kwa kusema kuwa TCB iko tayari kushirikiana na serikali, sekta binafsi na wananchi katika kuhakikisha dira hii haiishii kuwa maandiko tu, bali inatekelezwa kwa vitendo ili kuleta mabadiliko chanya kwa taifa.
“TCB iko mguu sawa katika kutekeleza dira ya 2050, na tutaendelea kuwa sehemu ya mageuzi ya uchumi wa Tanzania,” amesisitiza Mihayo.