Na Mwandishi wetu, Dodoma
KATIBU Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla amesema maandalizi ya mchakato wa uchaguzi ndani ya CCM yanaendelea vizuri na kikao cha mwisho cha uteuzi wa Wagombea kitafanyika July 28, 2025 ambapo Kamati Kuu ambayo ilikuwa ikae leo na kuteua Wagombea wa Ubunge na Udiwani kwenye kura za maoni imeahirisha kuketi leo.

Akizungumza leo July 19,2025 jijini Dodoma Makalla amesema sababu ya kuahirisha Kamati Kuu leo ni kutokana na majina ya Watia nia kuwa mengi na hivyo mchakato wa kuendelea kuyachambua ili kutenda haki unaendelea huku akisema kabla ya kikao hicho cha July 28,2025, kitafanyika pia kikao cha Halmshauri Kuu July 26,2025.
“Maandalizi ya mchakato wa uchaguzi ndani ya CCM unaendelea vizuri na kikao cha mwisho cha uteuzi wa Wagombea kitafanyika tarehe 28, ile Kamati Kuu ambayo ilikuwa iteue leo tarehe 19 kwahiyo uteuzi wa mwisho utafanyika tarehe 28 hapahapa Dodoma,”amesema.
“Leo wengi walitarajia Kamati Kuu itafanya kikao chake na kufanya uteuzi wa mwisho kwa walioteuliwa kugombea kwenye kura za maoni, Wagombea sasa watulie wakati tunaendelea na mchakato, unajua Wagombea wengi sana kwahiyo kazi ya kuchagua ni kubwa na sisi tunataka tutende haki na tuifanye vizuri kwahiyo watulie, wa-relax mpaka tarehe 28 uteuzi wa mwisho utafanyika na kwenda kwenye kura za maoni.
Niliona simu nyingi kwamba vikao vimeahirishwa mkawa mnanipigia simu nyingi sasa hii ndio taarifa ya Chama, Watia nia watulie,”amefafanua.