Home KITAIFA INEC yaasisitiza maandalizi ya Uchaguzi kuzingatia misingi ya sheria na maadili

INEC yaasisitiza maandalizi ya Uchaguzi kuzingatia misingi ya sheria na maadili

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesisitiza maandalizi ya Uchaguzi Mkuu yanafanyika kwa kuzingatia misingi ya sheria, maadili, na utulivu ili kuepusha malalamiko kutoka kwa wadau wa uchaguzi.

Akizungumza Julai 21 2025 katika ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu kwa waratibu wa uchaguzi, wasimamizi na maafisa kutoka mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, Mjumbe wa Tume hiyo, Balozi Omar Ramadhan Mapuri, amesisitiza kuwa utekelezaji wa majukumu ya uchaguzi unapaswa kuongozwa na Katiba, sheria, kanuni na miongozo ya Tume.

“Tunahitaji uchaguzi wenye amani, utulivu na unaoendeshwa kwa weledi wa hali ya juu. Hili linawezekana kama kila mmoja atasoma kwa kina na kuelewa nyaraka zote muhimu za uchaguzi, na kuuliza maswali pale panapotokea changamoto za uelewa,” amesema Balozi Mapuri.

Pia amewataka wasimamizi wa uchaguzi kuhakikisha wanatambua mapema vituo vya kupigia kura ili kupanga mahitaji mahsusi na kuhakikisha kuwa siku ya kupiga kura haina vurugu wala mkanganyiko.

Ameonya pia kuhusu tabia ya upendeleo katika uteuzi wa watendaji wa vituo vya kupigia kura, akisisitiza kuwa waajiriwe watu wenye sifa zinazostahili kama vile weledi, uzalendo, maadili na bidii ya kazi.

“Tusiingize ndugu na jamaa wasio na sifa. Uchaguzi ni suala nyeti linalohitaji uadilifu wa hali ya juu,” ameoonya.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga Kura wa Tume hiyo, Giveness Aswile amesema mafunzo hayo yalipangwa kufanyika awamu mbili ambapo awamu ya kwanza yalifanyika Julai,15 hadi 17 na awamu ya pili yanaendelea kufanyika kuanzia Julai, 21 hadi 23 mwaka huu.

Amesema mafunzo hayo kwa sasa yanawahusisha wasimamizi na waratibu wa mikoa ya Dar es Salaam, Pwani huku mikoa mingine inayoshiriki ikiwa Shinyanga, Kusini Pemba, Mwanza, Rukwa na Mbeya.

Mafunzo hayo yamejumuisha washiriki 106 na yanatarajiwa kumalizika Julai 23, 2025, yakilenga kuwajengea uwezo waratibu wa uchaguzi wa ngazi ya jimbo pamoja na wasimamizi na wasaidizi wa uchaguzi ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kwa mujibu wa sheria.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here