Na Amani Nsello- MOI
WATAALAMU wazawa zaidi ya 70 wamepewa mbinu za kisasa za kutoa matibabu kwa wagonjwa ili kupunguza madhara yatokananyo na dawa kwa wagonjwa nchini Tanzania.

Hayo yamebainishwa leo Julai 22, 2025 na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Dk. Hamad Nyembea, Wizara ya Afya kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya usingizi tiba na ganzi salama katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI).
Dk. Nyembea amesema kuwa kuwa serikali imechukua hatua madhubuti ya kuhakikisha matumizi ya usingizi tiba na ganzi salama unazingatiwa.

“Madhara yatokanayo na matumizi ya ganzi yasipodhibitiwa vizuri yanaweza kuhatarisha maisha ya mgonjwa… Hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha matumizi ya ganzi yanakuwa salama, sahihi na yanayozingatia viwango vya kitaalamu,” amesema Dk. Nyembea
Aidha, ameeleza kuwa kupitia ushirikiano kati ya Tanzania na India, madaktari wazawa watapata nafasi ya kwenda India kwa ajili ya kuongeza ujuzi zaidi kuhusu fani ya usingizi tiba na ganzi.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Balozi Dk. Mpoki Ulisubisya, amesema mafunzo hayo yamekusudiwa kutoa elimu ya vitendo kwa watoa huduma ili kuongeza ubora wa huduma kwa wagonjwa.

Kwa upande wake Katibu wa Shirikisho la Vyama vya Madaktari Bingwa wa Usingizi Tiba na Ganzi Duniani (WFSA), Dk. Balavenkata Bubramanian, ameipongeza Tanzania kwa juhudi zake katika kuboresha huduma za usingizi tiba na ganzi na kueleza kuwa WFSA itaendelea kushirikiana na nchi wanachama kutoa mafunzo, vifaa na msaada wa kitaalamu ili kuinua kiwango cha huduma hizo barani Afrika.