📍 TAZA kufungua biashara ya umeme kati ya Tanzania na Zambia
📍 MD Twange awataka wasimamizi wa mradi kuhakikisha muda wa kimkataba unazingatiwa
Na: Mwandishi Wetu, Iringa
MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Lazaro Twange, amefanya ziara ya kikazi tarehe 23 Julai 2025 kukagua maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Tanzania – Zambia (TAZA) katika Mkoa wa Iringa na Njombe maneo ya ujenzi wa njia ya umeme na vituo vya kupoza umeme vya Tagamenda na Kisada.

Katika ziara hiyo, Twange ametoa maelekezo kwa wasimamizi wa mradi kuhakikisha ujenzi wa njia za kusafirisha umeme pamoja na vituo vya kupokea, kupoza na kusambaza umeme unakamilika kwa wakati kama ilivyoainishwa kwenye mikataba, huku akisisitiza kuwa usimamizi thabiti ni muhimu ili kuleta tija na kuhakikisha wananchi wananufaika kwa wakati.
“Simamieni wakandarasi vizuri katika kutekeleza ujenzi wa miradi hii. Msisimamie kwa mazoea, bali kwa weledi na kasi ili tija ya miradi hii ionekane na wananchi wapate huduma kwa wakati,” amesisitiza Twange.
Aidha, ametumia fursa hiyo kuwapongeza wasimamizi kwa juhudi zinazofanyika hadi sasa licha ya changamoto zinazojitokeza katika usimamizi wa miradi mikubwa, aliwataka kuendelea kutumia kipindi hiki kisicho na mvua kufanya kazi kwa kasi ili mradi ukamilike kwa ufanisi kama ilivyopangwa na Serikali.

Katika ziara hiyo, Twange pia alitembelea miradi ya upanuzi wa vituo vya kupokea na kusambaza umeme katika Kituo cha Cotex (Iringa) na Kituo cha Makambako (Njombe), ambavyo tayari vimekamilika kwa kiasi kikubwa na kuanza kutoa huduma kwa wateja.
Ameeleza kuwa hali ya umeme katika mikoa hiyo sasa imeboreshwa kwa kiwango kikubwa, huku miundombinu ikiwa na uwezo mkubwa wa kuhudumia mahitaji ya sasa na ya baadaye.
“Nimefurahishwa na utekelezaji wa miradi hii ya vituo vya kupoza umeme katika mikoa ya Iringa na Njombe. Kwa sasa tuna uwezo mkubwa wa kuhudumia wateja wengi zaidi kuliko hapo awali,” ameeleza.

Akihitimisha ziara hiyo ya siku mbili, Twange alionesha kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa Mradi wa TAZA, ambapo hadi sasa ujenzi wa njia za kusafirisha umeme umefikia zaidi ya asilimia 60, na ujenzi wa vituo vya kupoza umeme upo kwenye asilimia 31. Alisisitiza dhamira ya TANESCO kuendelea kusimamia miradi kwa ufanisi ili kutimiza malengo ya kitaifa ya upatikanaji wa umeme wa uhakika.

Mradi TAZA ni sehemu ya mpango wa kuunganisha Tanzania na Zambia kwa njia ya umeme na unakusudiwa kufanikisha biashara ya umeme katika Ukanda wa Kusini mwa Afrika (Southern Africa Power Pool).