Na Mwandishi wetu, Dodoma
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, William Lukuvi ameonya Wakandarasi wanaosuasua kukamilisha ujenzi wa Majengo ya Wizara na Taasisi katika Mji wa Serikali Mtumba licha ya serikali kutoa fedha.

Waziri Lukuvi ameyasema hayo Julai,23 2025 Jijini Dodoma alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa majengo hayo ambayo yanagharimu Sh. biloni 738.
Ameagiza kuhakikisha wanakamilisha ujenzi huo kabla ya Oktoba mwaka huu ili watumishi waweze kuhamia na kutoa huduma kwa wananchi.

Waziri Lukuvi amebainisha kuwa hakuna kisingizio cha kusuasua kwa ujenzi huo kwani Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa fedha kwa ajili ya kukamilisha.
“Wasukumeni wakandarasi wanaosuasua kukamilisha ujenzi wa kudumu wa ofisi za wizara na taasisi ili watumishi wote wahamie na watoe huduma kwa wananchi, kama ilivyotakiwa na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa urahisi na wepesi,” amesisitiza Lukuvi.
Aidha, ameongeza kuwa, “Tunatamani baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu wizara zote ziwe zimehamia Mtumba ili kurahisisha utoaji huduma kwa wananchi.

Katika hatua nyingine Lukuvi amezipongeza wizara ambazo tayari zimeshahamia licha ya majengo yao kutokukamilika ikiwemo Wizara ya Afya, Wizara ya Katiba na Sheria na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Pia amesisitiza kila Wizara na Taasisi kuzingatia maelekezo yaliyotolewa ya ununuzi wa samani zinazotengenezwa nchini ili kujivunia vitu vinavyotengenezwa na wazawa kwani kwa kufanya hivyo kutachoche ukuzaji wa uchumi wa Taifa na kukuza uzalendo.
“Tunatamani kuona samani zote zitakazonunuliwa ziwe za kutoka Tanzania kama tulivyoelekeza katika mikataba yenu kwasababu tumebaini kuwa samani hizo zinadumu kwa muda mrefu,”amesema

Kwa Upande wake Mratibu wa Kikosi cha Kuhamishia Serikali Dodoma na Uendelezaji wa Mji wa Serikali Mtumba, Noel Mlindwa amesema ujenzi unahusisha majengo 34 ya wizara na taasisi za serikali ambapo hadi sasa ujenzi huo umefikia asilimia 92.2 hadi kukamilika kwake utagharimu Shilingi biloni 738.
Vilevile amesema hadi hivi sasa serikali imeshatoa shilingi.bilioni 544.7 kwa ajili ya sughuli mbalimbali za ujenzi.
“Hadi sasa hatua ya iliyofikiwa kwa ujumla kwa majengo yote 34 ni asilimia 92.2 ya ujenzi ambapo katika hayo ni majengo 10 ya wizara yameshakamilika na watumishi wamehamia na kuanza kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi”,amesema.
Amefafanua kuwa, Katika kuhakikisha mji unakuwa wa kijani wanatarajia kupanda miti 253,000 kuzunguka maeneo yote ya mji wa serikali.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA), Mhandisi Benjamini Maziku alisema ujenzi wa barabara kilometa 59.1 katika mji wa serikali Mtumba imekamilika kwa asilima 100.
Amesema pia ujenzi wa barabara hizo ulienda sabambamba na ufungaji wa taa za barabarani na kamera kwa ajili ya usalama.
“Zoezi la ufungaji wa taa za barabarani limekamilika kwa asilimia 100 hivi sasa tunaendelea na majaribio ya taa hizo kwasababu tuna mkataba wa miaka mitano na mkandarasi na zikileta shida anakuja kubadilisha,” amesema.