Na Esther Mnyika, Dar es Salaam
RAIS Dk.Samia Suluhu Hassan anatarajia kuzindua Kituo cha Biashara na Usafirishaji cha Afrika Mashariki (EACLC), kilichopo Ubungo, jijini Dar es Salaam Agosti Mosi mwaka huu.

Kituo hicho kina maduka zaidi ya 2000 na kinatajwa kuwa kitachochea ukuaji wa uchumi kupitia biashara na kuongeza mapato.
Akizungumza leo Julai, 31 2025 Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema uzinduzi wa kituo hicho ni uwekezaji wa kimkakati kati ya serikali na wawekezaji kutoka nchini China.

Amesema kituo hicho kina maabara, maegesho ya magari na ofisi za kisasa na kimejengwa kwa gharama ya dola za kimarekani milioni 100.
“Uwepo wa kituo hicho hautaathiri fursa za Watanzania, kwani serikali ilishawahi kufahya ubia katika ujenzi wa maeneo mengine kama Mlimaji City hivyo wawekezaji na Watanzania wote wanakaribishwa kufanya biashara,” amesema.
Ameeleza kuwa miaka michache iliyopita walihamisha stendi ya Ubungo kwenda Mbezi mwisho na utekelezaji wa kituo hicho ulianza Mei mwaka 2023 na umekamilika mwaka huu kwa asilimia 99.
Ametoa wito wawekezaji kuendelea kuwekeza nchini miradi yenye tija wafike kwa Mamlaka husika pia Watanzania wajitokeze kwa wingi kwenye uzinduzi huo.