Home KITAIFA Makamu wa Rais afungua maonesho ya Nanenane Kitaifa 2025

Makamu wa Rais afungua maonesho ya Nanenane Kitaifa 2025

Na Mwandishi wetu, Dodoma

MAKAMU wa Rais wa Dk. Philip Mpango ametoa rai kwa viongozi kutambua wajibu wa kuetekeleza Dira ya Taifa 2050 na mipango ya maendeleo ya sekta ya kilimo ambayo imedhamiria kuongeza kasi ya ukuaji wa kilimo hadi kufikia asilimia 10 kwa mwaka, ifikapo 2030 na kuendelea.

Ametoa rai hiyo leo Agosti, 1 2025 jijini Dodoma na Dk. Mpango wakati wa ufunguzi wa maonesho na sherehe za wakulima, wafugaji na wavuvi (Nanenane) zinazofanyika Kitaifa katika Viwanja vya Nzuguni mkoani.

Amesema viongozi ni vema kuwajibika kuwaelekeza wakulima, wafugaji na wavuvi kuweka nguvu zaidi kwenye mazao yenye thamani kubwa sokoni, kuwekeza katika uzalishaji wa kisasa ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje, kuvutia wawekezaji wa ndani na nje pamoja na kuwekeza katika miundombinu baridi ya uhifadhi na usafirishaji.

“Ni vema Viongozi kuhamasisha uwekezaji mkubwa katika teknolojia za kisasa za kilimo, ikiwemo kilimo-janja, uwekezaji katika umwagiliaji, upatikanaji wa fedha na mitaji,kutafuta masoko ya uhakika na kuhakikisha wanajiimarisha zaidi katika kilimo-biashara,”amesema.

Pia amesema ni inapaswa Viongozi kusimamia uwezeshaji wa wakulima, wafugaji na wavuvi kiuchumi, hususan upatikanaji wa mitaji, teknolojia, elimu na mafunzo, pamoja na upatikanaji wa huduma za ugani, ikiwemo kukuza matumizi ya kanuni bora za kilimo. Halikadhalika kuhamasisha maendeleo ya ushirika na ushirikiano kati ya wakulima,wafugaji,wavuvi na watafiti, maafisa ugani na watunga sera.

Dk. Mpango amesema ni wajibu wa viongozi kuhimiza wananchi kutumia mbinu zinazoweza kuhimili athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi na changamoto nyingine zinazowakumba wakulima ikiwemo kuhimiza matumizi bora ya ardhi, kushawishi wananchi kupanua mawanda ya kilimo na kuhimiza zaidi kilimo cha mazao yanayohimili ukame.

Ametoa wito wa Viongozi kutoa elimu kwa wakulima, wafugaji, wavuvi na wasindikaji wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi kuhusu fursa zilizopo za kupata mitaji kutoka kwenye Benki na Taasisi nyingine za fedha ambazo tayari zinatoa mikopo nafuu kwa ajili ya kilimo-biashara.

Amesema mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya kilimo nchini yametokana na juhudi mbalimbali za wakulima, wafugaji, wavuvi, wadau wa maendeleo, pamoja na jitihada mahususi za Serikali inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika kukuza sekta hiyo.

Amesema jitihada hizo ni pamoja na kuongeza bajeti za Wizara za Kilimo, Mifugo na Uvuvi, pamoja na sekta nyingine saidizi. Katika bajeti ya 2025/2026 Wizara ya kilimo imetengewa Shilingi Trilioni 1.243, ikilinganishwa na Shilingi Bilioni 229.99 mwaka 2021/2022. Vilevile, Wizara ya Mifugo na Uvuvi nayo imetengewa Shilingi Bilioni 476.6 ikilinganishwa na Shilingi Bilioni 169.2 mwaka 2021/2022. Hatua nyingine mahsusi ni pamoja na kuongeza upatikanaji wa ruzuku za pembejeo, kuimarisha upatikanaji wa mitaji na kuhimiza maendeleo ya ushirika, kuwezesha upatikanaji wa huduma za ugani na zana bora za kilimo, kujenga miundombinu ya kuhifadhi mazao na kutafuta masoko ya mazao na bidhaa za kilimo.

Akisoma hotuba kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego amesema Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na wadau itaendelea kutekeleza vipaumbele vya kilimo ikiwemo kuongeza tija za uzalishaji, kuchangia kuongeza ajira zenye ustaha pamoja na ushiriki wa vijana na wanawake katika sekta ya kilimo.

Ametaja hatua zingine zitakazosimamiwa na Wizara ni pamoja na kuimarisha usalama wa chakula na lishe, kuimarisha upatikanaji wa masoko, mitaji na mauzo ya mazao ya kilimo nje ya nchi. Pia kuimarisha maendeleo ya ushirika na kuimarisha matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika uendelezaji wa Sekta ya Kilimo.

Amesema Wizara imeendelea kuwashauri, kuwaelimisha na kuwawezesha wakulima kuzingatia sheria na maelekezo ya wataalam ya kutunza mazingira, kulinda vyanzo vya maji, kupanda miti na kuzingatia matumizi sahihi ya teknolojia za kilimo.

Maonesho ya Nanenane ya mwaka 2025 yanaongozwa na Kaulimbiu isemayo “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi 2025”. Kaulimbiu hii imechaguliwa mahsusi ili kukumbusha umuhimu wa viongozi bora katika kuinua uzalishaji kwenye kilimo, ufugaji na uvuvi, hasa katika kipindi kuelekea Uchaguzi Mkuu, Oktoba 2025.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here